1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya amani ya kimataifa ni finyu

Admin.WagnerD20 Februari 2017

Mkutano wa usalama wa Munich umemalizika kwa onyo la kuwepo kwa matumaini finyu ya kupatikana kwa amani ya kimataifa na utulivu huku suala la Syria likihodhi mkutano huo wa siku tatu.

https://p.dw.com/p/1HvXh
Mwenyekiti wa mkutano wa usalama wa Munich Wolfgang Ischinger.
Mwenyekiti wa mkutano wa usalama wa Munich Wolfgang Ischinger.Picha: Getty Images/L. Preiss

Wolfgang Ischinger mwenyekiti wa mkutano wa usalama uliofanyika mjini Munich Ujerumani akiiufunga mkutano wa usalama wa Munich amesema "Tunakabiliwa na mizozo chungu nzima na kama ilivyosemwa asubuhi kushindwa mara nyingi kwa utatuzi wa mizozo na kuzuwiya mizozo kwa uhakika.Tunakabiliana na ukosefu wa utulivu usiotabirika katika sehemu zaidi ya moja na tunakabiliana na idadi kubwa ya wakimbizi iliovunja rekodi na muhimu kuliko yote tunakabiliwa na kupoteza kwa imani."

Ameongeza kusema kwamba hakuna maafikiano makubwa yaliofikiwa kutokana na kuendelea kutiliana mashaka na kutoaminiana kati ya mataifa.Mzozo wa Syria ulihodhi agenda ya mkutano huo wa siku tatu.

Rais Barack Obama wa Marekani hapo jana ameihimiza Urusi kuacha kuwashambulia kwa mabomu waasi wa msimamo wa wastani nchini Syria katika juhudi za kumuunga mkono mshirika wake Rais Bashar al Assad mashambulizi ambayo mataifa ya magharibi inayaona kwamba ni kikwazo kikuu katika juhudi za karibuni kabisa za kukomesha vita nchini Syria.

Matumaini finyu

Mkutano wa usalama wa Munich nchini Ujerumani.
Mkutano wa usalama wa Munich nchini Ujerumani.Picha: Reuters/M. Dalder

Mataifa makubwa yamekubaliana hapo Ijumaa kupunguza uhasama nchini Syria lakini makubaliano hayo hayategemewi kuanza kazi hadi mwishoni mwa wiki hii na hayakusainiwa na makundi yoyote yale yanayohasimiana yaani serikali ya Syria na makundi mbali mbali ya waasi yanayoipinga serikali hiyo.

Mashambulizi ya anga ya Urusi dhidi ya makundi ya waasi yanalisaidia jeshi la Syria kufanikisha kile kitakachoweza kuwa ushindi wake mkubwa kabisa wa vita katika mapambano ya Allepo mji mkubwa kabisa nchini Syria na kitovu cha biashara cha nchi hiyo kabla ya kuanza kwa vita.

Hakuna matumaini makubwa kwamba makubaliano hayo yaliofikiwa Munich yatakuwa na uwezo mkubwa wa kukomesha vita vya miaka mitano vilivyouwa watu 250,000.

Urusi yatakiwa kusitisha mashambulizi

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Getty Images/AFP/J. Samad

Wakati mkutano huo ukimalizika zimekuja taarifa kwamba Rais Barack Obama wa Marekani na mwenzake Vladimir Putin wa Urusi wamekubaliana baada ya kuzungumza kmwa njia ya simu kuwa na ushirikiano wa karibu katika kusuhughulikia mzozo wa Syria na Ukraine na hiyo kutowa matumaini fulani ya kufanyika kwa juhudi za kidiplomasia kutatuwa mizozo hiyo.

Lakini taarifa ya Ikulu ya Urusi pia imeweka wazi kwamba nchi hiyo imejitolea katika mashambulizi yake dhidi ya Dola la Kiislamu na makundi mengine ya kigaidi ishara ambayo inaonyesha kwamba pia itayalenga makundi mengine yalioko magharibi mwa Syria ambapo wapiganaji wa jihadi kama vile kundi la Al Qaeda wanapambana na Assad wakiwa karibu na waasi wanaonekana kuwa wa msimamo wa wastani na mataifa ya magharibi.

Urusi inasema kundi la Dola la Kiislamu la lile la Al Nusra lenye mafungamano na Al Qaeda ndio yanayolengwa katika mashambulizi yake ya anga.Lakini mataifa ya magharibi yanasema kwa kweli Urusi kwa kiasi kikubwa inayalenga makundi mengine katika mashambulizi hayo yakiwemo yale inayoyaunga mkono.

Wananchi wa Syria watelekezwa

Riad Hjab kiongozi wa upinzani nchini Syria unaoungwa mkono na Saudi Arabia.
Riad Hjab kiongozi wa upinzani nchini Syria unaoungwa mkono na Saudi Arabia.Picha: picture alliance/Photoshot

Akizungumza katika mkutano huo wa Munich Waziri Mkuu wa zamani wa Syria na kiongozi wa ujumbe wa upinzani unaoungwa mkono na Saudi Arabia Riad Hijab amelaumu kusambaratika kwa mchakato wa kisiasa chini ya usimamizi wa kimataifa.

Amesema "Wananchi wetu wanaona wametelekezwa na kuangushwa na jumuya ya kimataifa na hususan mataifa makubwa yenye nguvu na hasa Marekani."

Watu wengi wanasema mkutano wa Munich umetuma ujumbe kwa dunia kwamba juhudi zaidi zinahitajika kutatua mizozo inayoendelea kufukuta katika nchi kama Syria ikiwa ni pamoja kujenga upya imani iliopotea pamoja na kuyapa nguvu mazungumzo ya kisiasa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman