1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya Erdogan yamwagiwa mchanga

5 Februari 2014

Ziara ya waziri mkuu wa Uturuki nchini Ujerumani, na hali nchini Ukraine ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/1B2vu
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Uturuki Erdogan wakati wa mkutano na waandishi habari mjini BerlinPicha: Getty Images

Tuanzie lakini Berlin ambako matumaini ya waziri mkuu wa Uturuki yalimwagiwa mchanga na kansela kabla ya kushangiriwa siku hiyo hiyo usiku na maelfu ya watu wenye asili ya Uturuki.Gazeti la "Neue Osnabrücker" linaandika:"Alishangiriwa kama mwimbaji nyota,waziri mkuu Erdogan na maelfu ya waturuki katika ukumbi wa Tempodrom mjini Berlin.Maendeleo yanawezekana tu akiwa yeye madarakani,ndio kauli mbiu.Mwanasiasa huyo anaejiiita "nahodha"alijimwaga kati kati ya umati wa waturuki waliokuwa wakimshangiria.Nje lakini ya jengo hilo wafuasi wa mashirika ya kituruki yanayompiga Erdogan waliandamana.:Erdogan sio tena shujaa ambae wengi walikuwa wakimfikiria.Mara anajitokeza kama muimla,mara mfuasi wa itikadi kali:Amejiharibia mwenyewe.Anauelewa vibaya mfumo wa taifa linaloheshimu sheria,anaamuru waandamanaji wakamatwe na watumishi wa vyombo vya sheria wahamishwe mahala kwengine.Kwa hivyo inaingia akilini na ni sawa kabisa kansela Angela Merkel alipoyamwagia mchanga matumaini yake ya kutaka Uturuki iwe mwanachama kamili wa umoja wa ulaya.

Maneno matupu hayatoshi

Hali nchini Ukraine pia inaendelea kumulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.Gazeti la Bild linahisi ;"Wanasiasa wa dunia hii wanamjua vilivyo Vitali Klitschko-lakini kumsaidia hawajamsaidia vya kutosha.Hata hivyo jana waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier ameionya serikali ya Ukraine itawekewa vikwazo.Bora hivyo kwasababu kuubembeleza utawala wa kiimla hakusaidii kitu.Rais Janukowitsch na wafuasi wake wanajitajirisha kwa jasho la wananchi.Anaelizusha hivi sasa suala la kukusanywa mabilioni ya fedha kuisaidia Ukraine atakuwa anafanya pupa.Kwasababu Janukowitsch amebainisha "hendi" bila ya shinikizo".Pekee vikwazo vya Umoja wa ulaya-mfano marufuku kwa wafuasi wa Janukowitsch kuingia katika nchi za umoja huo na kuzifunga akonti zao,ndivyo vitakavyoweza kweli kumsumbuwa.Serikali ya Marekani imeitambua zamani hali hiyo ndio maana inafuata njia hii ya pili.Hii ni njia pekee itakayowasaidia waandamanaji katika uwanja wa Maidan.Kwasababu haitoshi pekee kupiga picha pamoja na Klitschko na kumuahidi maneno matupu.Anahitaji matamshi bayana na vitendo dhabiti pamoja na msaada wa nchi za magharibi.

Ukraine Kiew Protest Menschenmasse Flaggen
Umati wa watu wamekusanyika katika uwanja wa Uhuru mjini Kiev nchini UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu