1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumizi ya kijeshi yameongezeka duniani kote

P.Martin10 Juni 2008

Matumizi ya kijeshi kote duniani yameongezeka kwa asilimia 45 katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita na nusu ya gharama hizo zimesababishwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/EGiq

Ripoti ya mwaka iliyotolewa na SIPRI yaani Taasisi ya Kimataifa ya Stockholm kuhusu Utafiti wa Amani inasema,mwaka jana peke yake matumizi ya kijeshi yaliongezeka kwa asilimia 6.Katika mwaka 2007,kiasi cha Dola bilioni 1,339 zilitumiwa kwa silaha na gharama zingine za kijeshi.Hiyo ni sawa na asilimia 2.5 ya pato la ndani la dunia nzima.Marekani ni taifa lenye matumizi makubwa kabisa ya kijeshi.Mwaka jana ilitumia Dola bilioni 547 yaani matumizi yake yalikuwa asilimia 45 ya matumizi yote ya kijeshi duniani.

Uingereza,China,Ufaransa na Japan ni nchi zingine zenye matumizi makubwa ya kijeshi,lakini gharama za kila nchi moja katika kundi hilo,ni kama asilimia 4 hadi 5 ya matumizi ya dunia nzima.Ripoti ya SIPRI inasema,sababu zinazochangia kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi ni shabaha za sera za kigeni za baadhi ya nchi,vitisho vya kweli au vinavyodhaniwa,migogoro ya mapigano na sera za kuchangia wanajeshi katika operesheni za kimataifa kulinda amani na bila shaka uwezo wao wa kiuchumi.

Ukuaji mkubwa umeshuhudiwa kanda ya Ulaya ya Mashariki,ambako matumizi ya kijeshi yaliongezeka kwa asilimia 162 kati ya mwaka 1998 na 2007 na kwa asilimia 15 kuanzia mwaka 2006 hadi 2007.Mwaka jana matumizi ya kijeshi ya Urusi yalipanda kwa asilimia 13 na kuchangia asilimia 86 ya gharama za kijeshi katika kanda hiyo.

Kwa upande mwingine,matumizi ya bara la Amerika ya Kaskazini yalifumuka kwa asilimia 65.Sehemu kubwa ya gharama hizo ilisababishwa na Marekani iliyoongeza matumizi yake kwa asilimia 59 kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Kwa upande mwingine,Mashariki ya Kati imeongeza matumizi yake ya kijeshi kwa asilimia 62 katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita:Eshia ya Kusini kwa asilimia 57 na Bara la Afrika kwa asilimia 51 sawa na nchi za Asia ya Mashariki.Ulaya ya Magharibi ni eneo pekee lililokuwa na ongezeko dogo kabisa katika matumizi yake ya kijeshi yaani kwa asilimia 6 tu.Amerika ya Kusini imeongeza matumizi yake ya kijeshi kwa asilimia 14.China,kwa kiwango cha kitaifa,imeongeza matumizi yake ya kijeshi kwa mara tatu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Ni dhahiri kuwa matumizi ya kijeshi yaliyoongezeka yamezidisha pia biashara ya makampuni mashuhuri 100 yanayotengeneza silaha duniani.Biashara hiyo iliongezeka kwa takriban asilimia 9 katika mwaka 2006 kulinganishwa na 2005 na ilifikia Dola bilioni 315.Kutoka makampuni hayo 100 mashuhuri ya silaha,63 yapo Marekani na Ulaya ya Magharibi.