1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumizi ya nishati mbadala yaongezeka duniani

Sudi Mnette
12 Januari 2024

Ripoti mpya ya Shirika la Kimataifa la uratibu wa Nishati (IEA) inaonesha kuwa mataifa ulimwenguni yameongeza asilimia 50 zaidi ya uwezo wa matumizi ya nishati mbadala isiyochafua mazingira mwaka 2023.

https://p.dw.com/p/4b6wC
Mkutano wa Dubai ulitoa shinikizo kwa baadhi ya nchi kuhusu matumizi ya nishati mbadala
Mkutano wa Dubai ulitoa shinikizo kwa baadhi ya nchi kuhusu matumizi ya nishati mbadalaPicha: Amr Alfiky/REUTERS

Mkutano wa kilele wa wa mazingira COP28 unaoongozwa na Umoja wa Mataifa ulihitimishwa huko Dubai mwezi uliopita na takriban mataifa 200 yalikubali wito wa kwanza kabisa kwa kujiondoa hatua kwa hatua kutoka katika matumizi ya nishati za visukuku.

Taaarifa ya shirika la IEA inasema "Kiasi cha uwezo wa nishati mbadala ulioongezwa kwenye mifumo ya nishati duniani kote kilikua kwa asilimia 50 mwaka 2023, na kufikia karibu gigawati 510, huku kile kiwango kilichochangiwa na nishati ya jua kikiongeza robo tatu ya nishati duniani kote."

''Nishati safi tayari kuongezeka kwa mara mbili ifikapo 2030''

Ripoti hiyo imesema China iliongoza juhudi hizo, kwa kutumia kiwango kikubwa cha nguvu za jua, ikilinganishwa na sehemu kubwa ya ulimwengu kwa mwaka 2022.

Aidha ripoti hiyo iliongeza kuwa uwezo wa  matumizi ya nishati katika mataifa ya Ulaya, Marekani na Brazil uliongezeka. Mkuu wa shirika hilo la IEA Fatih Birol amesema ripoti inaonesha "chini ya sera za sasa na hali ya soko, uwezo wa kimataifa wa nishati safi tayari uko katika mwelekeo wa kuongezeka kwa mara mbili na nusu ifikapo 2030".

Changamoto ya ufadhili kwa nchi zinazoendelea

Nchi zinazoendelea bado zakabiliwa na changamoto za miundombinu za nishati jadidifu
Nchi zinazoendelea bado zakabiliwa na changamoto za miundombinu za nishati jadidifuPicha: Bernat Armangue/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Hata hivyo amesema bado haitoshi katika kufikia lengo la COP28 la kuongeza mara tatu matumizi ya nishati hizo, lakini wako karibu na serikali zina zana zinazohitajika katika juhudi za kuziba pengo.

Birol amesema nishati ya upepo na nishati ya jua ni nafuu sasa kuliko mitambo mipya ya mafuta pamoja na mitambo iliyopo ya mafuta katika nchi nyingi.

Changamoto muhimu zaidi kwa jumuiya ya kimataifa kwa wakati huu ni jitihada za kuongeza kasi ya ufadhili na upelekaji wa bidhaa au mitambo katika nchi nyingi zinazoinukia na zinazoendelea kiuchumi ili ziweze kufanikisha mpango bora wa matumizi ya nishati safi.