1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya kuangamiza jamii Afrika ya Kati

12 Februari 2014

Mauaji ya kutokomeza jamii dhidi ya raia wa Kiislamu yanafanyika nchini Afrika ya Kati ambapo Shirika la Haki za Binaadamu la Amnesty International linasema wanajeshi wa kulinda amani wa kimataifa wanashindwa kuyazuwiya.

https://p.dw.com/p/1B7Fk
Wakimbizi wanaokimbia mashambulizi ya makundi ya dhidi ya balaka Afrika ya Kati.
Wakimbizi wanaokimbia mashambulizi ya makundi ya dhidi ya balaka Afrika ya Kati.Picha: 2013 Marcus Bleasdale/VII for Human Rights Watch

Amnesty imesema imeorodhesha takriban mauaji ya watu 200 ya raia wa Kiislamu yaliofanywa na makundi ya wanamgambo wa Kikristo yanayojulikana kama dhidi-ya balaka ambayo yaliundwa kufuatia mapinduzi ya mwezi wa Machi mwaka 2013 yaliofanywa na kundi la muungano wa waasi la Seleka lenye Waislamu wengi.

Katika repoti yake hiyo shirika la Amnesty limesema mauaji ya kuangamiza jamii ya Waislamu yamekuwa yakifanyika magharibi mwa nchi hiyo ambapo ndiko kwenye idadi kubwa ya wananchi wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa repoti hiyo jamii nzima za Kiislamu zimelazimika kukimbia na mamia ya raia wa Kiislamu ambao wameshindwa kukimbia wameuwawa na makundi ya wanamgambo ya dhidi ya balaka ambayo hayana uongozi mahsusi.

Shirika hilo limesema mashambulizi dhidi ya Waislamu kwa nia iliotamkwa wazi ya kuiondowa jamii yao nchini humo yanafanyika kutokanana wapiganaji wengi wa dhidi ya balaka kuwaona Waislamu kuwa wageni ambao wanapaswa kuondoka nchini humo au wauliwe.Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadaamu linaona kwamba makundi hayo yanafanikiwa kutimiza malengo yao hayo ambapo Waislamu wamekuwa wakilazimishwa kukimbia nchi hiyo kwa idadi inayoongezeka.

Wanamgambo wa makundi ya dhidi ya balaka Afrika ya Kati.
Wanamgambo wa makundi ya dhidi ya balaka Afrika ya Kati.Picha: picture-alliance/AP

Mfano mbaya

Amnesty imetowa wito kwa vikosi vya kulinda amani vya kimataifa vilioko nchini humo kuchukuwa hatua za haraka kukomesha udhibiti wa makundi ya dhidi ya balaka kwenye mtandao wa barabara wa nchi hiyo na kuweka wanajeshi wa kutosha kwenye miji ambapo Waislamu wako hatarini.

Pia imetaka vikosi hivyo vya kimataifa kupatiwa rasilmali zinazohitajika kufanikisha hayo na kuonya kutokea kwa maafa ya kishitoria yasio kifani ambayo yanaweza kuigwa na nchi nyengine zenye mizozo ya kidini au kikabila katika eneo hilo.

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa awali alivitaka vikosi vya kimataifa vilivyowekwa katika nchi hiyo yenye wakaazi wengi wa Kikristo kukomesha mashambulizi ya makundi hayo ya wanamgambo ikibidi hata kwa kutumia nguvu.

Nchi hatarini kugawika

Repoti hiyo ya Amnesty inakuja wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon hapo jana akielezea uwezekano kwamba nchi hiyo inaweza kugawika kutokana na mzozo wa umwagaji damu chini ya misingi ya kidini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki -moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki -moon.Picha: Getty Images/Pascal Le Segretain

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa kutaja uwezekano wa nchi hiyo ya kimaskini kugawika kati ya maeneno ya Waislamu na Wakristo.Matamshi yake yanaadamana na onyo kwamba hatua ya kimataifa kukabiliana na hali hiyo hailingani na uzito wa hali yeyewe na ameitaka dunia kuchukuwa hatua kutokana na kuongezeka kwa mauaji yanayofanyika kwa misingi ya kidini na ukosefu wa utawala wa sheria uliozagaa nchini humo.

Ametaka pia uangaliwe hata uwezekano wa kutumwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ziada ya wanajeshi 1,600 wa Ufaransa na wa 6,000 wa nchi za Kiafrika walioko nchini humo hivi sasa.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo