1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yaendelea nchini Syria

Josephat Nyiro Charo11 Juni 2012

Kiongozi mpya wa upinzani nchini Syria ameutaka Umoja wa Mataifa uchukue hatua madhubuti zinazoweza kutekelezwa kutumia nguvu ili kuwalinda raia kutokana na ukandamizaji unaofanywa na rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad.

https://p.dw.com/p/15Bsf
Free Syrian Army members raise their weapons during a training session on the outskirts of Idlib, Syria, Thursday, June 7, 2012. (Foto:AP/dapd)
Gewalt in SyrienPicha: dapd

Abdul-Basset Sida, ambaye alichaguliwa kama kiongozi mpya wa baraza la kitaifa la Syria kwenye mkutano uliofanyika mjini Istanbul nchini Uturuki, amezitaka dola kuu duniani kukomesha chombo cha mauaji nchini Syria chini ya ibara ya saba ya Umoja wa Mataifa. Sida amesema kama baraza la usalama haliwezi kufikia makubaliano, basi nchi zinaweza kuchukua hatua nje ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa.

Sida alikuwa mgombea pekee wa wadhifa huo wa miezi mitatu kwenye mkutano wa wanachama 33 wa sekretariat kuu ya baraza hilo. Baada ya kuchaguliwa kwake, ameyahakikishia makundi yote madogo nchini Syria, wakiwemo wakristo na Washia wa kabila la Alawi wanaowaogopa Wasunni, kwamba maisha yao yatalindwa na hakutakuwa na ubaguzi katika Syria mpya inayokuja.

Kiongozi huyo aidha amewataka wanachama katika serikali ya rais Assad wajiuzulu. Amesema kipindi muhimu kimeanza katika mzozo wa Syria uliodumu miezi 15 sasa, akiongeza kuwa serikali inakaribia kufika ukingoni na imepoteza udhibiti wa miji kadhaa.

Ngome za waasi zashambuliwa

Kauli ya kiongozi huyo imekuja wakati vikosi vya rais Assad vikifanya mashambulzi mapya ya kuudhibiti mkoa wa Homs. Wanaharakati wa upinzani wamesema watu wapatao 35 waliuawa jana kwenye mashambulizi ya maroketi na makombora yanayoelezwa kuwa mabaya zaidi tangu kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Aprili mwaka huu.

Ngome za upinzani katika mji wa Homs na Qusair, Talbiseh na Rastan katikati mwa Syria, zilishambuliwa. Vikosi vya Assad pia vilivishambulia vitongoji vya mji mkuu Damascus kujaribu kuwachakaza waasi ambao wamekuwa wakiimarisha mashambulizi karibu na ofisi za usalama mjini humo.

Uwezekano wa harakati ya kijeshi

Sambamba na hayo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza, William Hague, amedokeza kwamba hafutilii mbali uwezekano wa kuingilia kati kijeshi nchini Syria, akisema hali nchini humo inaanza kufanana na machafuko yaliyoikumbua Bosnia miaka ya 1990, ambapo maelfu ya watu waliuawa.

British Foreign Minister William Hague speaks at an Australian-British Chamber of Commerce lunch in Sydney, Wednesday, Jan. 19, 2011. Hague is visiting Australia for the Australia-United Kingdom Ministerial Consultations. (AP Photo/Rick Rycroft)
William Hague Außenminister GroßbritannienPicha: AP

Hague ameiambia televisheni ya Sky hapo jana kwamba muda unazidi kuyoyoma kuutekeleza mpango wa kusitisha mapigano uliopendekezwa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na wa jumuiya ya nchi za kiarabu kwa mzozo wa Syria, Kofi Annan, na kwamba Uingereza imeanza kutafakari hatua ya kuchukua iwapo mpango huo hautafua dafu.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/APE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef