1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yaendelea Syria, Brahimi akutana na upinzani

Admin.WagnerD14 Septemba 2012

Huku ghasia zikiendelea kutokea mjini Aleppo na Damascus, wachunguzi wa mambo wanafuatilia kwa karibu juhudi za mjumbe wa amani Lakhdar Brahimi kukomesha kadhia hiyo. Swali ni Je! Atakutana na Rais Bashar al- Assad?

https://p.dw.com/p/168rT
Moja ya ndege zinazotumiwa na Jeshi la Syria kushambulia waasi.
Moja ya ndege zinazotumiwa na Jeshi la Syria kushambulia waasi.Picha: Reuters

Mjumbe wa amani wa kimataifa, Lakhdar Brahimi, anatarajiwa kukutana leo na wajumbe wa upinzani nchini Syria, ambao wanavumiliwa na utawala wa Rais Bashar al- Assad. Pia, vikosi vya serikali ya Syria vimeushambalia mji wa Aleppo kwa kutumia ndege na helikopta za kijeshi, siku moja tu baada ya kutokea mauaji ya takriban watu 125 sehemu mbalimbali nchini humo.

Mashambulizi mjini Damascus yataisha lini?
Mashambulizi mjini Damascus yataisha lini?Picha: Reuters

Je! Brahimi atateta na Assad?

Wakati mkutano huo ukiwa umepangwa kufanyika mjini Damascus, bado hakuna taarifa za kuaminika iwapo Lakhdar Brahimi atakutana na Rais Bashar al- Assad.

Mpatanishi huyo ambaye aliwasili mjini hapo jana na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje, Walid al- Moallem, amesema mzozo wa kisiasa nchini humo unazidi kuwa mkubwa zaidi." Tunajua jinsi ilivyo vigumu, ni kama haiwezekani kabisa. Siwezi kusema haiwezekani, ni kama haiwezekani kabisa", alisema Brahimi.

Wapinzani wanadai kuwa kuwepo kwa Brahimi nchini Syria hakujaweza kukomesha machafuko kwani vikosi vya serikali bado vinaendelea kuishambulia miji ya nje ya Damascus, kama Yalda, kwa lengo la kuwafukuzia mbali waasi wanaotaka kuyachukua upya maeneo waliyoyateka awali.

Jana pekee takriban watu 190 wanakadiriwa kuuwawa katika maeneo mbalimbali nchini Syria, wengi wao ikiwa ni mjini Aleppo.

Damu itamwagika mpala lini?

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Haki za Binadamu la Syria, mashambulio hayo yalilenga miji ya Al- Bab na Marea, ambayo inashikiliwa na waasi karibu na mji wa Aleppo, huku makabiliano makali yakishuhudiwa katika uwanja wa ndege wa jeshi huko Minnigh

Mjumbe wa amani nchini Syria- Lakhdar Brahimi: Hali nchini Syria ni mbaya sana
Mjumbe wa amani nchini Syria- Lakhdar Brahimi: Hali nchini Syria ni mbaya sanaPicha: AP

Kwa wiki za hivi karibuni waasi wamefanya mashambulio yaliyolenga miji ya Deir Ezzor, Idlib na Aleppo, mji wa pili kwa ukubwa ambao ndio uwanja wa vita Kaskazini mwa Syria.

Msemaji wa shirika hilo, Rami Abdel Rahman, amesema askari wanaomtii Rais Bashar al- Assad wanazidi kuongeza silaha kupambana na waasi hao. Wanaharakati nao wamepanga kufanya maandamano mara tu baada ya sala za Ijumaa.

Jirani na mji mkuu wa Damascus, askari 15 wanahofiwa kuuwawa katika shambulio lililofanywa katika gari lao mjini Douma asubuhi ya leo, baada ya ghasia kuripuka katika jengo la manispaa.

Taarifa zaidi zinadai kuwa mjini Damascus kumesikika miripuko mikubwa mitatu usiku wa kuamkia leo.

Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul

Mhariri:Othman, Miraji