1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji yaendelea Yemen

19 Septemba 2011

Vikosi vinavyomtii Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen vimewapiga risasi na kuwauwa waandamanaji wengine 20 hivi leo (19.09.2011), na kufanya idadi ya waliouawa tangu jana kufikia 46, huku Umoja wa Mataifa ukitafuta suluhu

https://p.dw.com/p/12c61
Rais Ali Abdullah Saleh
Rais Ali Abdullah SalehPicha: picture-alliance/dpa

Mashahidi wameripoti kusikia milio ya risasi na mizinga katika mji mkuu, Sanaa, ambao umegawika baina ya upande wa wanaomuunga mkono Rais Saleh na wale wanaompinga.

Baba mmoja, ambaye mtoto wake amekufa kutokana na kupigwa risasi kichwani amesikikana akilia kwa uchungu huku akisema: "Ewe Mungu nisaidie, angalia haya mauaji. Tulikuwa kwenye gari katika mtaa wa Hayel. Nikashuka kuwanunulia watoto wangu wa kiume chakula. Mara nikasikia mkubwa akipiga makelele. Ndugu yake alikuwa amepigwa risasi ya kichwa".

Kwa mujibu wa mpasha habari wa Reuters, watunguaji walikuwa wakiwafyatulia risasi waandamanaji kutoka mapaa ya majumba. Baadhi ya vifo vinaonekana kusababishwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono.

Mauaji haya yametokea katika siku ambayo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Jamal bin Omar, na mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba, Abdullatif al-Zayani, wanawasili mjini Sanaa kutafuta muafaka wa kisiasa kati ya upinzani na serikali.

Mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba mpango wa Umoja wa Mataifa wa upatanishi umepangiwa kuwekwa saini Jumatatu ya leo.

Licha ya mauaji dhidi ya waandamanaji, maandamano dhidi ya Rais Saleh yamekuwa yakiendelea.
Licha ya mauaji dhidi ya waandamanaji, maandamano dhidi ya Rais Saleh yamekuwa yakiendelea.Picha: picture alliance/dpa

Kiongozi mwengine wa ngazi za juu wa Saudi Arabia ameliambia shirika hilo kuwa Makamo wa Rais wa Yemen, Abd-Rabb Mansour Hadi, ataweka saini mpango huo ulioandaliwa kwa ushirikiano na mataifa ya Ghuba ndani ya kipindi cha wiki moja, baada ya Marekani kusema kuwa inatarajia sana kuchukuliwa kwa hatua hiyo.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, Abubakr Abdullah Al-Qirbi amesema kwamba mauaji yaliyofanyika jana yatachunguzwa na serikali na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria. Al-Qirbi ametoa kauli hiyo leo, katika hotuba yake kwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, Uswisi.

Kauli hii ya Al-Qirbi imekuja baada ya Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Kyung-wha Kang, kuilaumu hadharani serikali ya Yemen kwa mauaji haya.

"Tunaitolea wito serikali ya Yemen kuacha mashambulizi dhidi ya raia na sehemu zinazokaliwa na raia, kwa mujibu wa wajibu wa Yemen chini ya Sheria za Kimataifa za Haki za Binaadamu". Alisema Kang.

Rais Ali Abdullah Saleh ameendelea kubakia nchini Saudi Arabia alikokwenda mwanzoni mwa mwezi Juni kutibiwa, baada ya Ikulu yake kushambuliwa, lakini hadi sasa amekuwa akiukataa mpango wa mataifa ya Ghuba wa kuwachia madaraka, na ambayo ni madai makubwa ya waandamanaji.

Kukataa kwake kumewakasirisha majirani zake wa Ghuba, ambao wanaamini kuwa kuendelea kwa ukosefu wa usalama nchini Yemen, kutarutubisha makundi yenye mafungamano na Al-Qaida katika eneo lao.

Makubaliano hayo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Ghuba, kama yatasainiwa, yatamfanya Rais Saleh awachie madaraka yake yote, na yeye na familia yake kupatiwa kinga ya kutoshitakiwa.

Mtoto wake, Ahmed Ali Saleh, ndiye anayeongoza kikosi maalum cha Republican Guard, ambacho kinatajwa kuhusika na mauaji kadhaa ya waandamanaji yakiwemo ya jana na leo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo