1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauritania yatakiwa iheshimu katiba

Hamidou, Oumilkher21 Oktoba 2008

Umoja wa Afrika na umoja wa Ulaya wawashinikiza watawala wa kijeshi wa mjini Nouakchott

https://p.dw.com/p/FeDm
Kiongozi wa utawala wa kijeshi jenerali Ould Abdel AzizPicha: DW / DPA



Umoja wa Afrika na Umoja wa ulaya "wanafuata msimamo wa aina moja,linapohusika suala la kuheshimiwa katiba nchini Mauritania"-Matamshi hayo yametolewa na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya,Jean Ping.


"Msimamo wetu unalingana kabisa na ule wa Umoja wa Ulaya kuhusu hali nchini Mauritania.Tunataka kuona katiba inaheshimiwa katika nchi hiyo ambayo wanajeshi wamepindua serikali na kunyakua madaraka Agosti sita iliyopita."Ameshadidia mwanasiasa huyo .


Mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Mauritania,jenerali Mohamed Ould Abdel Aziz amepuuza miito ya Umoja wa ulaya ya kutaka katiba iheshimiwe,na kusema  jana usiku "nchi yake haitorejea tena nyuma".


Kwa mujibu wa Jean Ping,Umoja wa Afrika umewapa muda watawala wa kijeshi na Umoja wa Ulaya umefanya hivyo hivyo ,kwa kutoa muda wa mwezi mmoja katiba iheshimiwe."Ni pendekezo la Paris kwa niaba ya Umoja wa ulaya-amesema mwenyekiti huyo wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika.


Jana Umoja wa ulaya umewapatia viongozi wa kijeshi wa Mauritania muda wa mwezi mmoja watoe mapendekezo ya namna ya kuanza kuheshimiwa katiba,la sivyo watakabiliwa na vikwazo.


Masharti hayo ya Umoja wa Ulaya yametajwa tena mwishoni mwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Mauritania ulioongozwa na waziri mkuu aliyeteuliwa na wanajeshi Moulaye Ould Mohamed Laghdaf na wawakilishi wa Umoja wa ulaya,jana usiku mjini Paris.


Umoja wa ulaya umelalamika kutokana na ile hali kwamba mapendekezo ya Mauritania hayazungumzii juu ya kuachiwa huru haraka na bila ya masharti ,rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia Sidi Ould Cheikh Abdallahi.Umoja wa Ulaya unahisi pia mapendekezo hayo hayaambatani na misingi ya katiba na hayatoi matumaini ya kuheshimiwa katiba.


September 22 iliyopita,Umoja wa Afrika uliwashinikiza viongozi wa kijeshi wa Mauritania wamrejeshe madarakani rais Ould Cheikh Abdallahi hadi ifikapo october sita ,la sivyo watakabiliwa na balaa la vikwazo na kutengwa pia.


"Awamu ya pili kwetu sisi ni kuliarifu baraza la usalama na ulinzi la Umoja wa Afrika kuhusu hali namna ilivyo tangu onyo lilipotolewa,na kuendelea kushauriana papo kwa papo na jumuia ya kimataifa".Baraza la usalama na ulinzi ndilo litakalopitisha uamuzi wakati huo."Amesema bwana Jean Ping.


Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa ulaya ambae hakutaka jina lake litajwe amesema awamu ya pili,baada ya viongozi wa kijeshi kupuuza muda uliowekwa itakua kulitaka baraza la usalama la umoja wa mataifa liiwekee vikwazo Mauritania.


Ubalozi wa Marekani mjini Nouakchott ulitangaza October 17 iliyopita kwamba serikali ya Marekani imewawekea vizuwizi vya kuingia Marekani baadhi ya watawala wa kijeshi na wa serikali pamoja na wote wanao waunga mkono.