1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauritania yumkini kupata msaada wa mataifa magharibi kupiga vita ugaidi

Mohamed Dahman24 Septemba 2008

Utawala wa kijeshi uliolaaniwa vikali tokea kuingia madarakani mwezi uliopita unaweza kupatiwa msaada wa mataifa ya magharibi kupiga vita ugaidi kufuatia shambulio baya la kundi lenye uhusiano na Al Qaeda nchini humo.

https://p.dw.com/p/FNsF
Mji mkuu wa Algiers Algeria umekuwa ukiathiriwa mara kwa mara na mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Kiislam la Maghreb kaskazini magharibi mwa Afrika kama inavyonekana hapo pichani katika shambulio karibu na Mahkam ya Katika mwaka 2007 ambapo watu kadhaa waliuwawa.Picha: AP

Wanajeshi 11 wa Mauritania na raia mmoja ambao walikuwa hawajulikani walipo kufuatia shambulio kwa doria yao kaskazini mwa nchi hiyo hapo tarehe 14 mwezi wa Septemba walipatikana wakiwa wamekatwa vichwa.

Kutekwa kwao nyara kulidaiwa kufanywa na tawia la Al Qaeda huko Afrika kaskazini katika taarifa kwenye tovuti inayodhaniwa kutoka kwenye kundi hilo na serikali ya Mauritania imesema shambulio hilo limefanywa na kundi hilo.

Kundi hilo ambalo linajiita kuwa Al Qaeda katika eneo la Kiislam la Maghreb linashukiwa kufanya mashambulizi katika eneo hilo zima la Afrika Kaskazini na kuvuta nadhari ya mataifa ya magharibi.

Isselmou Ould Moustapha mhariri mkuu wa gazeti la kila wiki nchini Mauritania la Tahalil Hebdo anasema utawala wa kijeshi umedhoofishwa na shambulio hilo ni shambulio la kijeshi na jeshi limedhalilishwa.

Hata hivyo kwa upande mwengine amesema pia umeimarishwa kwa sababu ya kuhurumiwa kwa wahanga.

Ameongeza kusema kwamba utawala huo wa kijeshi utataka kuhurumiwa na kuungwa mkono na mataifa ya magharibi ambayo yanakuwa na hisia nyeti sana kwa tishio la kigaidi na mara nyingi yanakuwa tayari kuridhia muafaka kusaidia serikali zinazokabiliwa na itikadi kali za Kiislam.

Kufuatia shambulio hilo Ufaransa imepongeza kujizatiti kikamilifu kwa taifa hilo katika vita dhidi ya ugaidi kunakofanywa na jeshi bila ya kuutaja kwa jina utawala wa kijeshi.

Ufaransa mkoloni wa zamani wa taifa hilo la kaskazini magharibi mwa Afrika ilikuwa imeongoza kulaani kimataifa kwa mapinduzi ya kijeshi ya Augusti 6 ambayo yamempinduwa kiongozi wa kwanza kabisa aliechaguliwa kidemokrasia nchini humo.

Jumapili iliopita Umoja wa Ulaya ulitowa taarifa kulaani shambulio hilo na kuelezea mshikamano katika vita dhidi ya ugaidi.

Mbali na Ufaransa wafadhili wengine wakuu wa Mauritania, Umoja wa Ulaya na Marekani pia walilani mapinduzi ya mwezi uliopita yasiokuwa na umwagaji damu ambayo yalimpinduwa Rais Sidi Ould Cheikh Abdallahi.

Zimetowa wito wa kurudishwa kwa utawala wa katiba na rais kuachiliwa kutoka kizuizi cha nyumbani lakini baadhi ya watu wanasema shambulio la Septemba 14 linaweza kusaidia kubadili sauti hiyo ya kidiplomasia.

Shambulio hilo litaimarisha hoja za utawala wa kijeshi kwamba jumuiya ya kimataifa haipaswi kuiwekea vikwazo au kuitenga nchi hiyo kwa sababu hali ya usalama inaendelea kuwa dhaifu anasema hayo Alain Antil mtafiti katika Taasisi ya Kifaransa ya Uhusiano wa Kimataifa.

Duru za kidiplomasia zimedokeza kwamba fikra ya jumuiya ya kimataifa yumkini tayari imeanza kubadilika.

Mwanadiplomasia mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba huu ni wakati mgumu kwa Mauritania lakini hawapaswi kukaa kimya bila ya kuchukuwa hatua kwa kisingizio hawautambuwi utawala huo wa kijeshi.

Wiki iliopita Umoja wa Ulaya ulimwalika kiongozi wa utawala huo wa kijeshi Generali Mohamed Ould Abdel Aziz kwa mazungumzo kuhusiana na hali iliosababishwa na mapinduzi hayo na mkutano huo huenda ukafanyika katika wiki ya pili ya mwezi wa Oktoba.

Hadi hivi karibuni kabisa Mauritania ilikuwa haikuathiriwa na mashambulizi ya kigaidi kukatwa vichwa kwa wanajeshi hao katikati ya mwezi wa mfungo wa Ramadhan kumezusha mawimbi ya fadhaa nchini kote Mauritania.