1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawakili wataka kesi ya Kenyatta ifutwe ICC

Admin.WagnerD11 Oktoba 2013

Mawakili wa rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wameomba kufutwa kwa kesi inayomkabili rais huyo na makamu wake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa madai ya kutishiwa kwa mashahidi katika kesi hiyo.

https://p.dw.com/p/19xzO
Rais wa Uhuru Kenyatta.
Rais wa Uhuru Kenyatta.Picha: John Muchucha/AFP/Getty Images

Katika barua yao yenye kurasa 38 iliyowasilishwa na mawakili wa rais Uhuru Kenyatta wamedai kuwa kuna ushahidi wa kutosha kutoka upande wa washitakiwa wa kutumiwa vibaya utaratibu wa mahakama hiyo ambao umejionyesha wazi kwa njia mbalimbali yakiwemo mazungumzo yanayofanywa kwa njia ya simu.

Aidha mawakili hao wametoa wito kusikilizwa moja kwa moja kwa kesi ikiwa itashindakana kufutwa wakidai kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka waliosaidia kupatikana kwa ushahidi na kuibua mashahidi zaidi katika kesi hiyo pia wanatishiwa na watu wasiofahamika.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda.
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda.Picha: Bas Czerwinski/AFP/GettyImages)

Kufuatia hali hiyo Kenya imeitaka mahakama hiyo kuifutilia mbali kesi hiyo au kuihamisha na kusikilizwa katika mahakama iliyo karibu na nchi hiyo. ICC hadi sasa inasikiliza kesi dhidi ya viongozi wa Afrika pekee.

Azidi kukana mashtaka
Kenyatta, ambaye alichaguliwa kuiongoza Kenya mwanzoni mwa mwaka huu, anakana mashitaka hayo ambapo mawakili wake wamesisitiza kusema kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka wanatoa ushahidi wa uongo. Wakati Rais Kenyatta akitakiwa kufika mbele ya mahaka hiyo Mwezi Novemba mwaka huu, Ruto alifikishwa katika mahaka hiyo mwezi uliopita.

Ikiwa kesi hiyo itasikilizwa hata hivyo rais Kenyatta huenda asihudhurie kutokana na kuiomba mahakama awali kwamba asihudhurie wakati kesi hiyo itakapokuwa ikisikilizwa ili aweze kuendelea na shughuli zake kama kiongozi wa ngazi za juu wa Kenya.

Waendesha mashitaka wa mahakama hiyo wanatarajiwa kujibu kwa maandishi ikiwa watakubali ombi hilo na kutoa mwongozo wa namna ya kuanza kusikiliza madai hayo. Rais Kenyatta na makamu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya kuandaa machafuko baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo mamia ya watu waliuwawa.

Ruto anatuhumiwa kupanga baadhi ya machafuko yaliyozuka baada ya uchaguzi mwaka 2007 ambapo watu wapatao 1,200 waliuwawa na zaidi ya 600,000 kupoteza makaazi yao.

Makamo wa rais wa Kenya, William Ruto.
Makamo wa rais wa Kenya, William Ruto.Picha: Michael Kooren/AFP/Getty Images

'Mashahidi wanatishiwa'
Kwenye maombi ya kuataka kufutwa kwa kesi hiyo, mawakili wa rais Kenyatta wamedai kuwa mashahidi wanatishiwa ili watoe ushahidi wa uongo, sambamba na kutishiana wenyewe kwa wenyewe na kuna kikundi cha waendesha mashitaka wanaotoa rushwa ili kumkandamiza rais Kenyatta.

Wiki iliyopita mahakama hiyo ilitoa amri ya kukamatwa kwa raia wa Kenya, mwandishi wa habari Walter Barasa, anayedaiwa kutakaka kupokea rushwa kuwahonga waendesha mashahidi wa Kenya ili wasitoe ushahidi.

Uchaguzi wa 2007 nchini Kenya uliandamwa na madai ya wizi wa kura na mizengwe, lakini kile kilichoanza kama ghasia za kisiasa kikageuka kuwa wimbi la mauaji ya kikabila na mashambulizi ya kulipiziana kisasi, yakiwa machafuko mabaya kabisa tangu uhuru wa nchi hiyo 1963.

Suala la Kenya kutaka kufutiwa kesi yake limekuja siku chache tu kabla ya Umoja wa Afrika kukutana kujadili ikiwa Nchi za Afrika zitajiondoa katika mahaka hiyo.

Mwandishi: Flora Nzema/APE/RTRE
Mhariri: Josephat Charo