1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri na wabunge wazidi kujiuzulu Peru

Sylvia Mwehozi
28 Desemba 2017

Rais wa Peru Pedro Pablo Kuczynski anazidi kukabiliwa na mgogoro juu ya uamuzi wake wa kumsamehe dikteta wa zamani Alberto Fujimori. Hadi sasa mawaziri wawili na wabunge kadhaa wamejiuzulu. 

https://p.dw.com/p/2q3bP
Peru Staatschef Pedro Pablo Kuczynski
Picha: picture alliance/dpa/Presidencia/Agentur Andina

Waziri wa utamaduni Salvador Der solar ametangaza uamuzi wa kujiuzulu jana Jumatano wakati Peru ikijiandaa kwa maandamano makubwa dhidi ya msamaha uliotolewa kwa rais wa zamani Alberto Fujimori. Tangazo la kujiuzulu kwake limekuja katikati mwa ongezeko la mgogoro wa kisiasa uliochochewa na uamuzi wa rais Pedro Pablo Kuczynski wa kumpatia msamaha Fujimori siku ya Jumapili.

Fujimori alikuwa amefungwa kwa ukiakaji wa haki za binadamu na alikua amelazwa hospitali mwishoni mwa juma. Msamaha huo ulikuja siku tatu baada ya rais Kuczynski kuepuka kura ya kutokuwa na imani naye ambayo mtoto wa Fujimori aliye mbunge Kenji, aliongoza uasi ambao haukutarajiwa dhidi ya kura hiyo, na kuleta ukosoaji kwamba kulikuwa na makubaliano baina yao.

Screenshot Video Facebook Alberto Fujimori
Alberto Fujimori rais wa zamani wa Peru aliyesamehewaPicha: Facebook

Waziri mkuu Mercedes Araoz alikataa madai hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jana Jumatano akisema uamuzi huo haukuwa wa siku moja kwani rais amekuwa akifuatilia afya ya Fujimori kwa muda sasa. Kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri na wabunge waziri mkuu anasema "Maafisa waliochukua uamuzi wa kujiondoa katika nyadhifa zao, hayo ni maamuzi yao na nayaheshimu. Hata hivyo nataka kusisitiza kwamba wengi wa mawaziri walikuwa waaminifu kwa rais na kwangu na kujiuzulu kwao kumefanyika kwa uaminifu kamili, lakini ninaelewa msimamo wao. Watu wengi wamejaribu kujipatanisha na dhamira zao lakini wamepata ugumu, kwahiyo nafikiri ninapaswa kuheshimu maamuzi yao."

Wanachama watatu wa chama tawala pia nao wamejiuzulu juu ya suala hilo, pamoja na mkurugenzi wa ofisi ya haki za binadamu ya wizara ya sheria . Waziri wa mambo ya ndani Carlos Basombrio alitangaza kujiuzulu kwake siku ya Ijumaa, hata kabla ya tangazo la msamaha kutolewa. Wakati huo huo wawakilishi wa baadhi ya wahanga wa utawala wa Fujimori wameiomba mahakama ya haki za binadamu ya Amerika ya Kusini, kubatilisha msamaha huo wa rais wa zamani.

Peru - Proteste nach Begnadigung von Fujimori
Polisi nchini Peru akipambana na waandamanajiPicha: Reuters/M. Bazo

Maandamano makubwa ya kupinga kusamehewa kwa Fujimori yamepangwa kufanyika leo mjini Lima. Fujimori ambaye ana uraia wa nchi mbili Japan na Peru, alitumia muda wake nchini Japan na kisha kuingia Chile, ambako alikamatwa mwaka 2005. Aliitawala Peru kutoka mwaka 1990 hadi 2000 kabla ya kukimbia makosa makubwa ya rushwa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Baada ya kurejeshwa kutoka Chile mwaka 2007 na kufungwa kwa miaka sita kwa matumizi mabaya ya madaraka, alipewa kifungo kingine cha miaka 25 jela kwa makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu aliyoyatenda wakati wa utawala wake, ikiwemo kuamuru mauaji ya watu 25.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa

Mhariri: Daniel Gakuba