1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa EU wakubaliana kuinusuru Euro

18 Mei 2010

Mawaziri wa Fedha kutoka nchi zinazotumia sarafu ya Euro, wametangaza kuchukua hatua za kukabiliana na hatari ya kushuka thamani kwa sarafu hiyo

https://p.dw.com/p/NQcL
Waziri Mkauu wa Luxembourg ambaye ni rais wa eneo la Euro Jean Claude Juncker, kulia akiwa na kamishna wa EU anayehusika na uchumi Olli Rehn katika mkutano na waandishi wa habari hii leoPicha: AP

Katika kikao chao kilichofanyika mjini Brussels, mawaziri hao pia wametangaza kuwepo kwa mazungumzo zaidi ili kukamilisha mpango wa kuwa na mfuko mkubwa wa fedha wa kusaidia nchi wanachama kukabiliana na madeni.

Mwenyekiti wa kikao cha mawaziri hao wa fedha wa nchi hizo za sarafu ya Euro,Waziri Mkuu wa Luxembourg Jean-Claude Juncker ameunga mkono mipango hiyo.

Miongoni mwao ni ule unaozitaka nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwasilisha rasimu ya bajeti zao katika makao makuu ya kamisheni ya umoja huo, kabla ya kupitishwa na mabunge ya nchi zao.

Hata hivyo, Bwana Jean-Claude Juncker amesisitiza kuwa, kamisheni hiyo haitakuwa msimamizi wa kutoa amri dhidi ya sera za bajeti kwa nchi wanachama.

Baadhi ya nchi ikiwemo Sweden zimeelezea kutokubaliana na mpango huo.Uingereza pia inategemewa kupinga kutokana na msimamo wa serikali mpya ya Waziri Mkuu David Cameron wa chama cha Conservative.

Siku nane zilizopita Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa ulitangaza mpango wenye thamani ya Euro billioni 750 kwa ajili ya mfuko utakazisaidia nchi wanachama wa umoja huo zenye madeni makubwa.

Pamoja na mpango huo, halikadhalika tangazo la wiki iliyopita kutoka nchi za Ureno na Uhispania, la kupunguza matumizi katika sekta ya umma ili kurejesha imani katika masoko ya fedha, lakini sarafu ya Euro iliendelea kuporomoka dhidi ya dola.

Hata hivyo Waziri Mkuu huyo wa Luxembourg alisema kuwa pamoja na kuporomoka kwa sarafu hiyo lakini bado ni imara.

EU Griechenland Finanzkrise Jean Claude Juncker Luxemburg
Jean Claude Juncker )Picha: AP

´´Tuna imani kuwa Euro ni sarafu inayoaminika.Kupanda kwa bei za bidhaa kumethibitiwa katika eneo la Euro kwa kipindi cha zaidi ya miaka 11 na kutaendelea kudhibitiwa katika miaka ijayo.Sarafu ya Euro ni mustakhabali muhimu kwa Ulaya na ni rasilimali kubwa kwa wawekezaji´´

Aidha Jean-Claude Juncker amesema kuwa, mpango wa kuanzishwa kwa mfuko huo wa mabilioni ya Euro kwa ajili ya kuzipiga jeki nchi wanachama zitakazokabiliwa na hali mbaya ya madeni,unahitaji mazungumzo zaidi ambayo yamepangwa kufanyika Ijumaa ijayo.Amesema kuna masuala ya kiufundi ambayo yanatakiwa kujadiliwa

Ujerumani nchi yenye uchumi mkubwa kabisa barani Ulaya, imesema kuwa ni lazima kwa nchi wanachama wa eneo la Euro kupunguza nakisi za bajeti zao katika kukabiliana na wasi wasi wa kuyumba kwa uchumi.Waziri wa Fedha wa nchi hiyo,Wolganga Schäauble alisema

Steuerschätzung Schäuble
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: picture-alliance/dpa

´´Ni lazima tupunguze nakisi.Tunahitaji kuimarisha mkataba wa Umoja wa Ulaya.Bilashaka ni lazima leo tulizungumzie hilo ni vipi tunaweza kuimarisha ukuaji wa uchumi.Lakini kupunguza nakisi katika bajeti, hilo ni jukumu ambalo kila mmoja lazima alitekeleze kwa ajili yake binafsi na kwa ajili ya wote´´.

Ujerumani ndiyo nchi iliyochangia kiwango kikubwa cha fedha katika mpango wa kuikopesha Ugiriki kukabiliana na deni kubwa iliyonalo.Ugiriki leo hii inapokea kiasi cha Euro billioni 14.5 za dharura kati ya Euro billioni 110 ilizoahidiwa kupewa na nchi za eneo la Euro pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF katika kipindi cha miaka mitatu.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Josephat Charo