1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

041011 Euro-Gruppe Luxemburg

4 Oktoba 2011

Ugiriki itabidi isubiri hadi kuweza kupatiwa fungu jipya la mkopo wa Euro bilioni nane. Mawaziri wa fedha wa nchi za eneo la sarafu ya Euro wamekubaliana jana usiku wasubiri kwanza kabla ya kupitisha uamuzi wao.

https://p.dw.com/p/12lEv
Picha: dapd

 Mawaziri hao wanasubiri kuona ripoti ya tume ya pande tatu inayozileta pamoja Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa, IMF. Hali hiyo haimaanishi lakini kwamba Ugiriki haina uwezo wa kulipa madeni yake.

Kimoja ni dhahiri: Ugiriki haitoweza kupunguza nakisi ya bajeti yake kwa kiwango kikubwa kama ilivyoahidiwa hapo awali. Serikali ya Ugiriki tayari imeshaungama. Nae kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya sarafu, Olli Rehn, akawaarifu mawaziri wa umoja wa sarafu ya Euro mara tu mkutano wao ulipoanza na kusema "Yadhihirika kana kwamba Ugiriki haitalifikia lengo lake mwaka huu."

Euro-Gruppen-Präsident Jean-Claude Juncker warnt vor Übergreifen der Euro-Krise
Rais wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Jean-Claude Juncker.Picha: picture-alliance/dpa

Ikiwa Ugikiri itashindwa kuyafikia malengo yaliyowekwa ambayo ni pamoja na kupunguza nakisi ya bajeti yake, huenda basi fungu jengine la mkopo lisitolewe. Hayo yalisemwa pia na waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani aliyesisitiza, hata hivyo, hakuna bado kilichoamuliwa,  wanasubiri ripoti ya tume ya pande tatu inayozileta pamoja Umoja wa Ulaya, Benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa, IMF.

Wakati huo huo, maandamano yanaendelea nchini Ugiriki. Watumishi wa serikali wamezifunga hii leo njia za kuingilia katika wizara  za fedha, kilimo na wizara nyengine kadhaa mjini Athens wakilalamika dhidi ya hatua za kufunga mikaja wanazohoji zinaukaba uchumi wa nchi hiyo.

Maandamano haya yanatokea mnamao  mkesha wa mgomo jumla wa masaa 24 ulioitishwa na shirika linalopigania masilahi ya wafanyakazi wa mashirika ya umma na yale ya kibinafsi.

Euro-Finanzminister diskutieren Rettungsschirm
Baadhi ya mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro.Picha: AP

"Watu wameingiwa na wasi wasi mkubwa na kukasirika sana" , amesema hayo Ilias Iliopoulos ambaye ni katibu mkuu wa shirika linalopigania masilahi ya watumishi wa mashirika ya umma-Adedy- anaeshiriki katika maandamano mbele ya wizara ya fedha.

"Maandamano ya leo yanahusiana na sheria za kazi. Lakini kuna bajeti mpya inayoashiria hatua ziada za kufunga mkaja-", ameongeza kusema Ilias Iliopoulos.

Mawaziri wa fedha wa nchi za eneo la sarafu ya Euro wametangaza jana Athens inaweza kusubiri hadi kati kati ya mwezi wa November mwaka huu kuweza kupata fungu jengine la mkopo wenye thamani ya Euro bilioni nane.

Muda huo unaweza ukatumiwa na tume ya pande tatu ili kuzidi kuishinikiza Ugiriki isawazishe mgogoro wake wa madeni.

Waziri wa fedha wa Ugiriki anatazamiwa kuzungumza na waandishi habari muda mfupi kutoka sasa.

Mwandishi: Hasselbach, Christoph(DW Brüssel)/Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri: Miraji Othman