1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Ulaya wakutana Brussels

Josephat Charo14 Mei 2007

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamekutana hii leo mjini Brussels, Ubelgiji. Viongozi hao wametoa mwito mapigano nchini Somalia yamalizike na kuahidi kupeleka misaada ya kiutu kuwasaidia Wasomali.

https://p.dw.com/p/CHEQ
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya hii leo wametaka mapigano baina ya vikosi vya serikali ya mpito ya Somalia na wanamgambo wa kiislamu yakome. Aidha mawaziri hao wameahidi kuongeza misaada ya kiutu kuwasaidia Wasomali wengi wanaoteseka kutokana na vita lakini kiwango kipya cha fedha zitakazotolewa hakikutajwa.

Mkutano wa Brussels umewataka wadhamini wa kimataifa wawajibike kuongeza misaada ya kiutu na juhudi za kuijenga upya Somalia. Wameitaka pia serikali ya mpito ya Somalia iondoe vikwazo vyote vinavyozuia usambazaji wa misaada ya kiutu na usafiri wa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada nchini Somalia.

Umoja wa Ulaya umesema unaunga mkono kuundwa kwa tume maalumu ya Umoja wa Afrika ya kulinda amani nchini Somalia. Umezitaka nchi nyengine duniani ziunge mkono juhudi za kuleta amani ndani ya Somalia na pande zinazohusika katika mzozo wa Somalia zijizuie kutokana na malumbano na zisitishe mapigano.

Umoja wa Ulaya umezishutumu pande mbili zinazohusika katika mgogoro wa Somalia kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kusisitiza kwamba mgogoro huo unaweza tu kutanzuliwa kupitia juhudi za kisiasa. Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wameyataka makabila yote ya Somalia yafanye mdahalo wa maana wa kitaifa.

Kabla kuanza kwa mkutano wa mjini Brussels wajumbe wa makundi ya kijamii kutoka Afrika, eneo Karibik na Pacific, wametoa mwito kuwepo biashara huru baina ya Umoja wa Ulaya na bara la Afrika.

Kuhusu amani ya Mashariki ya Kati, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema mchakato uliofufuliwa na jumuiya ya nchi za kiarabu unatakiwa upewe nafasi ili uweze kufaulu.

´Palestina inahitaji kuhakikishiwa kwamba mazungumzo ya amani hatimaye yatasababisha kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina, ambalo litaishi kwa amani sambamba na Israel. Israel nayo kwa upande wake inahitaji usalama na kutokuwepo kwa mashambulio.´

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamepangwa kukutana na wenzao wa jumuiya ya nchi za kiarabu mjini Brusssels baadaye leo katika juhudi mpya za kuundeleza mpango wa kutafuta amani katika Mashariki ya Kati.

Sambamba na hayo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ataondoka kesho kwenda Moscow kujaribu kuokoa mkutano baina ya Urusi na Umoja wa Ulaya usivunjike. Mkutano huo unatarajiwa kujadili hatua ya Urusi kukataa nyama kutoka Poland isiuzwe katika masoko yake.

´Kitendo hicho kimeufanya mkutano baina ya Umoja wa Ulaya na Urusi kuwa mgumu. Kuna matatizo mengi yanayotakiwa yatatuliwe ambayo yanaufanya mkutano huo kuwa mgumu.´Katika hali ambapo hali imekuwa ngumu, ni jambo la busara kukaa pamoja na kujadiliana.´

Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi pia utazungumzia hali ya baadaye ya jimbo la Kosovo.