1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakutana mjini Brussels

5 Machi 2007

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels kuzunguzumzia masuala kadhaa ikiwa pamoja na Iran, Darfur na ulinzi wa mazingira.

https://p.dw.com/p/CB5R
Javier Solana
Javier SolanaPicha: AP

Kwenye mkutano huo mawaziri hao wanatarajiwa kujadili mkakati wa kuimarisha vikwazo dhidi ya Iran baada ya nchi hiyo kukutaa kwa mara nyingine kutekeleza uamuzi wa baraza ,la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kuacha mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium.

Mawaziri hao pia wanajaribu kutafuta njia ya kuepusha mgongano unaoweza kusababishwa na misimamo tofauti juu ya suala la mazingira kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za Umoja wao unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

Nchi za Umoja wa Ulaya zinatofautiana juu ya kiwango cha kuwajibika katika dhima ya ulinzi wa mazingira.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wao wa mjini Brussels leo pia watazungumzia mgogoro wa Darfur magharibi mwa Sudan.

Kwa muda wa miaka kadhaa suala hilo limekuwa katika ajenda ya mawaziri hao hasa kwa kutambua kwamba mauaji bado yanaendelea katika jimbo hilo.

Kwenye mkutano wao mawaziri hao wanatarajiwa kusisitiza ulazima wa kuongeza shinikizo dhidi ya serikali ya Sudan ambayo hadi sasa imekuwa inapinga maamuzi kadhaa ya jumuiya ya kimataifa juu ya kutatua mgogoro wa Darfur.

Pamoja na hayo nchi za Umoja wa Ulaya zitatilia maanani ulazima wa misaada kuendelea kutolewa kwa maalfu ya watu wa Darfru waliolazimika kuyakimbia makao yao kutokana na mashambulio yanayofanywa na wanagambo .

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya pia wanatarajiwa kusisitiza ulazima wa kuendelea kuunga mkono na kuimarisha juhudi za kulinda amani katika jimbo la Darfur .

Kwenye mkutano wao leo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine watajadili njia za kufufua mchakato wa kuleta amani katika mashariki ya kati kwa kutilia maanani serikali ya umoja ya mamlaka ya Palestina baina ya vyama vya Hamas na Fatah.