1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

130309 EU Außenminister Treffen

Aboubakary Jumaa Liongo16 Machi 2009

Baraza la Mawaziri wa Nje wa Umoja wa Ulaya linakutana leo, Jumatatu, mjini Brussels, Ubeligiji.

https://p.dw.com/p/HDHi

 Kazi moja wapo kuu ni kutayarisha mkutano wa viongozi wa nchi na serikali kutoka Umoja wa Ulaya. Mkutano huo wa kilele utafanywa tarehe 19 hadi 20 mwezi huu wa Machi mjini Brussels chini ya kivuli cha mzozo wa kiuchumi.


Nchi nyingi katika Umoja wa Ulaya, kwa sehemu fulani, zimezindua mipango ya kufufua uchumi ambayo ni mzigo mkubwa kwa bajeti ya taifa. Kwa hivyo, nchi nyingi kwa hivi sasa zikijikuta katika hali hiyo ngumu zinapinga kutoa msaada mkubwa zaidi kama Rais wa Marekani Barack Obama anavyotaka.

Hata Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imependekeza kuanzisha mpango wao wenyewe kutokana na bajeti ya umoja huo katika jitahada ya kufufua uchumi uliodorora. Lakini hapo pia serikali nyingi zina wasiwasi na kile kitakachofanywa hasa na fedha zitakazotolewa kwa mpango unaotazamiwa kuanzishwa. Wakati huo huo, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, ameonya kutokuwa na matumaini makubwa hivyo.

"Bajeti ya Umoja wa Ulaya ni chini ya asilimia 1 ya pato la jumla la uchumi wa Ulaya.Kwa hivyo, sehemu muhimu ipo katika mikono ya nchi wanachama na itabakia hivyo kwa siku zijazo. Kwa hivyo, tusiwe na matarajio tusiyoweza kutimiza." amesema.


Mpango wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya hasa unazingtia kuwekeza katika miradi ya mazingira, nishati na miundo mbinu. Na miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na nchi wanachama na kufanikiwa, kwa mfano, nchini Ujerumani ni marupurupu yanayolipwa kwa magari ya zamani yanayofanywa kuwa vyuma baada ya mtu kuamua kununua gari jipya. Lengo la mpango huo ni kuzuia biashara kuporomoka zaidi na kusaidia viwanda vya magari.

Mada zingine zitakazojadiliwa na Baraza la Mawaziri leo hii mjini Brussels ni ulinzi wa mazingira, hali ya Mashariki ya Kati pamoja na uhusiano na nchi za Balkan ya Magharibi zinazotaka kuwa karibu zaidi na Umoja wa Ulaya. Upande wa mazingira,suala ni makubaliano kupatikana miongoni mwa nchi za umoja huo kabla ya mkutano muhimu kabisa wa mazingira utakaofanywa mwisho wa mwaka huu. Wajumbe kutoka takriban mataifa 200 watakutana katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen, kwa matumaini ya kukamilisha mkataba mpya wa mazingira. Mkataba huo wa kimataifa utachukua nafasi ya Mkataba wa Kyoto baada ya mwaka 2012.


Mwandishi: Hasselbach, C. /P.Martin 

Mhariri: MIraji Othman