1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Ulinzi wa Sudan, S. Kusini wajadili usalama

Admin.WagnerD4 Juni 2012

Mawaziri wa Ulinzi kutoka Sudan na Sudan Kusini walikutana Jumatatu katika kikao maalum mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili masuala yanayohusu usalama katika mipaka ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/157oU
This photo of Saturday, April 14, 2012, shows Sudan Peoples Liberation Army (SPLA) troops at their position in the Unity Oil Field near to the front lines at Heglig, South Sudan. Two Sudanese Sukhoi fighters dropped 6 bombs in the Bentiu area, killing five and wounding four others. (AP Photo / Michael Onyiego)
Sudan Südsudan Soldaten in der Nähe von HegligPicha: AP

Mkutano huu unafuatia kuanza upya kwa majadiliano baina ya pande hizi mbili yaliyokuwa yamevunjika hapo awali kutoka chokochoko zilizokaribia kuzipeleka Sudan mbili katika vita. Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini John Kong na mwenzake Abdelrahman Mohamed Hussein wa Sudan anayetafutwa na mahakama ya Kimataifa, ICC waliongoza kikao hicho.

Mkutano huo umezungumzia uanzishwaji wa taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhakiki wa pamoja mipakani, mfumo wa ufuatiliaji na uanzishwaji wa kanda salama isiyokuwa na shughuli za kijeshi katika mpaka baina ya nchi hizo.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir.Picha: picture-alliance/dpa

Wajumbe kutoka pande zote wamefanya vikao kadhaa mjini Addis Ababa baada ya kunaza upya kwa majadaliano haya yaliyosimama tangu kutokea kwa mapigano ya mpakani kwenye maeneo yanayogombaniwa wiki kadha zilizopita, yaliyotishia kutokea kwa vita vikubwa.

UN, AU watoa muda wa mwisho kwa Sudan, S.Kusini kufikia mwafaka
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wamezipa Sudan mbili muda hadi kufikia Agosti 2 wawe wameshapata suluhu juu ya mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuainisha mpaka wa kila moja, usafirishaji wa mafuta na masuala ya uraia. Wakati wa kufunga siku ya tano ya tano ya mazungumzo haya yanayoongozwa na Umoja wa Afrika, kiongozi wa mjadala kwa upande wa Sudan Kusini Pagan Amum aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa pande mbili zilikubaliana kutekeleza mpango wa amani wa AU na UN.

Tunafurahi kuwa pande husika na paneli ya mazungumzo wamekubali kutekeleza kikamilifu azimio nambari 2046 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mpango wa Umoja wa Afrika, alisema Amum. Lakini aliikosoa Sudan kwa kutaka kuweka masharti kabla ya kuendelea kwa mazungumzo kamili na kuongeza kuwa Sudan ilikuwa inasisitiza juu ya mjadala wa usalama kabla ya mambo mengine yote.

Alisema serikali ya Sudan ilikuwa inajaribu kulaazimisha agenda fulani ya usalama ijadiliwe kwanza na kuongeza kuwa hilo lilikuwa ni sharti la kabla ambalo ni ukiukwaji wa mpango wa amani wa Umoja wa Afrika na pia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit.
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit.Picha: picture alliance / ZUMA Press

Abyei kujadiliwa Juni 7
Amum alisema kuwa paneli ya usuluhishi ya Umoja wa Afrika iliitisha mkutano tarehe 7 Juni kujadili jimbo la Abyei ambalo limekuwa chanzo kikuu cha uhasama baina ya Sudan na Sudan Kusini. Alisema pande mbili zitajadili uanzishwaji wa utawala na mifumo mingine muhimu kwa urejeshaji wa amani jimboni humo.

Duru ya sasa ya mazungumzo ilifunguliwa wiki iliyopita huku Sudan Kusini ikiishtumu Kaskazini kwa kukataa kuondoa majeshi yake kutoka Abyei. Umoja wa Mataifa ulikuwa umezipa nchi hizo hadi Mei 16 kuondoa majeshi yao kutoka Abyei lakini Sudan haikuondoa majeshi yake hadi tarehe Mosi Juni.

Sudan na Sudan Kusini zilipigana vita vya muda mrefu zaidi katika historia ya bara la Afrika kabla ya kutengana Julai mwaka jana huku Juba ikichukua sehemu kubwa ya vyanzo vya mafuta.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.