1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mawaziri watishia kujiuzulu Israel

27 Machi 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametoa wito wa umoja na kulaani machafuko yanayoendelea nchini humo.

https://p.dw.com/p/4PK5t
Israel Protest gegen die Justizreform
Picha: Ilan Rosenberg/REUTERS

Netanyahu ameutoa wito huu huku nchi hiyo ikiwa imegubikwa na maandamano yanayopinga mageuzi yenye utata katika idara ya mahakama, mgomo mkuu wa wafanyakazi wa umma na jeshi ambalo liko katika tahadhari.

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter Jumatatu, Netanyahu amewataka waandamanaji nchini humo kutoka mirengo yote ya kushoto na kulia kuwajibika na kutozua vurugu akisema wote ni ndugu.

Waziri Mkuu huyo alitarajiwa kutoa hotuba ambayo ingerushwa moja kwa moja katika televisheni mapema Jumatatu ili kutangaza mipango ya mabadiliko katika idara ya mahakama ambayo anasema yanahitajika ili kuleta usawa katika mfumo wa serikali, ila hotuba hiyo imeahirishwa.

Mawaziri watishia kujiuzulu

Hotuba hiyo imeahirishwa kwa kuwa Netanyahu amekutana na wakuu wa vyama katika serikali yake ya muungano.

Israel Protest gegen die Justizreform/Netanjahu im Parlament
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa katika KnessetPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Katika mkutano huo, Netanyahu anaripotiwa kujadili kuhusiana na uwezekano wa kuusimamisha mchakato huo wa mageuzi ya mahakama.

Ripoti zinaarifu kwamba mawaziri kadhaa katika serikali yake wametangaza kwamba watajiuzulu kutoka kwenye nafasi zao iwapo Netanyahu atatangaza kuusitisha mchakato huo.

Waziri wa sheria Yariv Levin ambaye amekuwa akiongoza mchakato huo amesema kama mwanachama wa chama tawala cha Likud, ataunga mkono uamuzi wowote atakaoufikia Netanyahu kama waziri mkuu.

Mgomo ulioitishwa Jumatatu na chama cha wafanyakazi nchini Israel chenye wanachama laki nane, umeathiri pia usafiri wa kimataifa katika uwanja wa ndege wa Tel Aviv huku makumi kwa maelfu ya watu wakitarajiwa kuathirika na mgomo huo na mabadiliko ya safari za ndege.

Kiongozi wa muungano wa wafanyakazi katika uwanja huo wa ndege wa Ben Gurion, Pinchas Idan, amesema ameamrisha usafiri wa ndege kusitishwa mara moja.

Mgomo huo umeathiri pia sekta za afya na benki miongonimwa sekta zengine. Wafanyakazi katika balozi za Israel katika nchi tofauti pia walisusia kazi.

Maandamano nje ya Knesset

Huku wabunge wakikutana bungeni, maelfu ya waandamanaji wamejitokeza kwa mara nyengine mitaani, wengi wakipeperusha bendera za Israel ambazo zimekuwa kama nembo ya maandamano hayo.

Israel Protest gegen die Justizreform Jair Lapid
Kiongozi wa upinzani Yair Lapid akiwahutubia waandamanaji nje ya KnessetPicha: Hazem Bader/AFP

Lakini wanaounga mkono mageuzi hayo katika idara ya mahakama wamejikusanya na kufanya maandamano mbele ya bunge la Knesset. Maandamano hayo yamejumuisha kundi moja la wafuasi wa klabu moja ya mpira mjini Jerusalem, liitwalo La Familia ambalo ni kundi linaloshabikia klabu ya Beitar Jerusalem.

Huku kukiwa na hofu ya machafuko inayochochewa katika mitandao ya kijamii ambapo kunatolewa miito ya kuwashambulia Waisraeli wa siasa za mrengo wa kushoto, idadi ya polisi imeongezwa ili kukabiliana na vurugu zinazoweza kutokea.

Chanzo: DPA/Reuters