1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May apoteza wingi wa viti bungeni

Yusra Buwayhid
9 Juni 2017

Chama cha Conservative cha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kimepoteza wingi wa viti bungeni baada ya uchaguzi wa Alhamis ulioitishwa mapema na May kuelekea mazungumzo ya Brexit ya kujiondoa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2eMmM
Großbritannien Wahlen 2017 - Theresa May
Picha: Getty Images/C. J. Ratcliffe

Wapigakura nchini Uingereza wamempiga dafrau kubwa waziri mkuu wao kwa kumkosesha ushindi wa moja kwa moja kuweza kuunda serikali ya chama chake cha Conservative. 

Hata hivyo, kwa kuwa hakuna mshindi wa wazi wa uchaguzi huo wa jana (Juni 8), May ameashiria kwamba huenda akabakia kwenye nafasi yake ya uwaziri mkuu, akiongoza serikali isiyokuwa na wingi wa kutosha bungeni. 

Mpinzani wake, Jeremy Corbyn wa chama cha Labour, amemtaka May ajiuzulu na ampishe kuunda serikali. Wachambuzi wa mambo wanasema uamuzi wa May kuitisha uchaguzi wa mapema, zaidi ya miaka miwili kabla ya wakati, lilikuwa kosa, na pia kampeni zake zilikuwa na mapungufu makubwa.

Kati ya viti 647 kwenye 650 vilivyotangazwa, Conservative imejikingia viti 316, pungufu ya viti kumi kuweza kuunda serikali yenye wingi bungeni. Labour kimepata viti 261. 

Uwezekano wa serikali ya mseto

UK Parlamentswahlen- PK des Labour-Parteichefs Jeremy Corbyn
Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama cha upinzani Labour, anamtaka May ajiuzulu. Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Brady

Awali ilitabiriwa kwamba chama cha Waskochi, Scottish National, kingelipata viti 32 na chama cha Liberal Democrats viti 11 bungeni. Sasa ama May au Corbyn watapaswa kushirikiana na moja vyama hivyo kuunda serikali ya pamoja au wenyewe kwa wenyewe.

Aidha inaripotiwa kwamba, thamani ya pauni ambayo ni sarafu ya Uingereza ilianguka kwa zaidi ya senti mbili ilinganishwa na dola ya Kimarekani, mara tu baada ya kutangazwa matokeo hayo, lakini baadaye ilipanda kidogo.

Jumla ya wabunge 650 wamepigiwa kura katika uchaguzi wa jana katika taifa la watu milioni 45.8 wenye haki ya kupiga kura.

Ili chama kimoja kiweze kuunda serikali kinahitaji kushinda viti 326 katika bunge la Uingereza. Chama cha Conservative kilikuwa na viti 330 katika bunge lililomalizika, ikilinganishwa na viti 229 vya chama cha Labour, 54 vya chama cha Scottish National na viti tisa vya Liberal Democrats.

Kwa vyovyote vile, matokeo ya uchaguzi huu yanamfedhehesha May aliyetisha uchaguzi wa mapema kwa matumaini ya kukiongezea wingi wa viti bungeni chama chake cha Consevative ili Uingereza iwe na nguvu katika mazungumzo yajayo ya Brexit ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba