1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May kuanza mchakato wa Brexit mwishoni mwa Machi

2 Oktoba 2016

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema Jumapili (02.10.2016) ataanza mchakato wa kujitowa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa Machi kwa mara ya kwanza akiashiria ratiba ya talaka kwa sura mpya ya uhusiano na umoja huo.

https://p.dw.com/p/2QoVs
England Premierminsterin Theresa May
Picha: Getty Images/C. Court

Kura ya fadhaa ya Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya hapo mwezi wa Juni ndio iliopelekea May kuingia madarakani na tokea wakati huo waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani amekuwa kwenye shinikizo kutowa ufafanuzi zaidi kuhusu mpango wake wa kuondoka kwa Uingereza katika umoja huo ziada ya kauli mbiu yake anayoitumia mara kwa mara kwamba "Brexit inamaanisha Brexit " yaani kujitowa kwa Uingereza katika umoja huo inamaanisha kujitowa sio venginevyo.

Katika hatua ya kutuliza hofu miongoni mwa wanachama wenzake wa chama cha Conservative kwamba huenda akachelewesha talaka hiyo , May anatarajiwa kuuleza mkutano wa chama chake huko Birmingham katikati ya Uingereza kwamba amenuwia kusonga mbele na mchakato huo na kupata mkataba unaofaa.

Kwa kutumia kifungu nambari 50 cha Mkataba wa Lisbon uliounda Umoja wa Ulaya kutaipa Uingereza kipindi cha miaka miwili kujipatia mkataba ambao unatazamiwa kuwa mmojawapo wa mkikataba migumu kufikiwa barani Ulaya tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

May amekiambia kipindi cha televisheni cha BBC kwamba"Tutanza kukitumia kifungu hicho kabla ya mwisho wa mwezi wa Machi mwakani."Amesema "Kutokana na sasa wanajuwa kuhusu wakati wa kufanya hivyo ....nataraji hilo litatuwezesha kuwa na matayarisho fulani ili kwamba inapokuja kuanza kukitumia kifungo hicho mchakato wa mazungumzo uwe mwepesi.

Kujitowa kwa Uingereza kunazusha hofu

England Premierminsterin Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.Picha: Getty Images/C. Court

Uamuzi wa Uingereza kujitowa Umoja wa Ulaya hapo Juni 23 ulisababisha msukosuko katika masoko ya fedha pale wawekezaji walipojaribu kupima taathira ya hatua hiyo kwa pande zote mbili uchumi wa nchi hiyo ambao unashika nafasi ya tano duniani na kwa Umoja wa Ulaya wenyewe.

Washirika wa nchi hiyo wanahofu kwamba kujitowa kwake huko Umoja wa Ulaya kunaweza kuanzisha sura mpya katika masuala ya kimataifa ya kipindi cha baada ya Vita Baridi ambayo itadhoofisha mataifa ya magharibi katika kukabiliana na China na Urusi,kuyumbisha juhudi za muungano wa Ulaya na kuathiri biashara huru ya dunia.

Sarafu ya pauni ya Uingereza ilishuka na kufikia kiwango ambacho hakikuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 31 na hivi sasa inabadilishwa kwa centi 40 za Kimarekani au asilimia 25 chini ya kiwango cha juu ilichokuwa nacho kwa miaka sita ambapo kilifikia kilele katikati ya mwaka 2014.

Athari za kujitowa

Großbritannien Treffen Theresa May und Martin Schulz
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akizungumza na Rais wa Bunge la Ulaya Martin Schulz.Picha: picture alliance/AA/British Prime Ministry

Hatua hiyo ya kuanza kutumia kifungu cha kuanza mchakato huo wa kujitowa itaonyesha kwamba ameazimia kufanikisha Brexit licha ya kufanya kampeni ingawa sio ya nguvu kubwa kwa Uingereza kuendelea kubakia Umoja wa Ulaya.

Wabunge wake wengi wanaona tangazo hilo limekuja kwa wakati kwamba wapiga kura watakuwa wamefahamu kuwa waziri mkuu huyo mpya alikuwa akihitaji muda zaidi kuuandaa msimamo wake.Wengine wanasema wanahofu kwamba kuanza kutumika kifungu nambari 50 na mapema kungeliweza kuweka shinikizo kwa Uingereza kutokana na kwamba uchaguzi nchini Ujerumani na Ufaransa mwaka 2017 kunaweza kukabidili washirika wa Uingereza katikati ya mazungumzo hayo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters

Mhariri : Sekione Kitojo