1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazishi yaandamana na ghasia Lebanon

22 Oktoba 2012

Polisi Lebanon wamepambana na waandamanaji wakati wakijaribu kuivamia ofisi ya waziri mkuu mjini Beirut huku kukiwa na wito wa kumtaka ajiuzulu baada ya mripuko wa bomu kwenye gari kumuuwa afisa mwandamizi wa usalama.

https://p.dw.com/p/16ULW
Mazishi ya Wissam
Mazishi ya WissamPicha: Reuters

Polisi ilifyetuwa risasi hewani na kutumia gesi ya kutowa machozi kuvunja maandamao yaliofuatia baada ya mazishi ya Generali Wissam al Hassan hapo jana.Tukio hilo limetumiwa kama fursa ya kupinga hatua ya Syria kuingilia mambo ya Lebabon lakini ghafla hali ikabadilika na hasira zakaelekezwa kwa Waziri Mkuu Najib Mikati ambaye serikali yake inadhibitiwa na vyama vyenye kuiunga mkono Syria kama vile Hizbullah na washirika wake.

Zaidi ya maafisa usalama 15 wamejeruhiwa katika mapambano na waandamanaji nje ya Serail ambayo ni ofisi ya waziri mkuu.Wakati wa kutowa rambi rambi za mkuu huyo wa ujasusi yaliyeuwawa,  waziri mkuu wa zamani aliekuwa na hasira Fuad Siniora amemtaka Mikati ajiuzulu na kuongozea sauti yake kwa nyengine nyingi ,tokea kuuwawa kwa Hassan na watu wengine wawili pamoja na kujeruhiwa kwa watu 126 hapo Ijumaa.

Marehemu Wissam Al Hassan mkuu wa ujasusi nchini Lebanon.
Marehemu Wissam Al Hassan mkuu wa ujasusi nchini Lebanon.Picha: picture-alliance/dpa

Siniora mwanachama mwandamizi wa kundi la upinzani la waziri mkuu wa zamani Saad Hariri amesema serikali inawajibika kwa kifo cha Hassan na dereva wake na kwamba inapaswa kuachia ngazi.Polisi mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba takriban vijana 200 walielekea kwenye jengo la waziri mkuu katikati ya jiji la Beirut lakini vikosi vya usalama viliwazuia kwa kufyetuwa risasi hewani na kutumia gesi ya kutowa machozi.

Masaa machache baada ya mazishi hayo yaliofanyika katikati ya Beirut,milio mizito ya risasi ilisikika kutoka eneo linalokaliwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni magharibi ya Beirut.Licha ya wito wa kumtaka ajiuzulu,Mikati amesema ataendelea kubakia madarakani kufuatia ombi la Rais Michel Suleiman ili kuepusha pengo la madaraka katika nchi tete ya Lebanon.Mikati amesema amemuelezea rais wasi wasi wake kutokana na kile kinachotokea nchini na amemthibtishia kwamba han'gan'ganii wadhifa wa uwaziri mkuu na kwamba ni jambo muhimu kuangalia suala la kuunda serikali mpya.

Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati anayekabiliwa na shinikizo la kujiuzulu.
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati anayekabiliwa na shinikizo la kujiuzulu.Picha: AFP/Getty Images

Upinzani umekuwa ukimlaumu Rais Bashar al Assad wa Syria kwa shambulio la Ijumaa lililotokea kwenye eneo linalokaliwa na Wakristo wengi la Ashraffieh.Upinzani pia unasema Assad anawajibika na mauaji ya baba wa Hariri, waziri mkuu wa zamani Rafik Hariri alieuwawa katika mripuko mkubwa wa bomu lililotegwa kwenye gari hapo mwaka 2005.Kumekuwepo na ghasia katika mji wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon, ngome ya Wasunni wakati wa usiku wa kuamkia leo ambapo upinzani dhidi ya Assad ni mkubwa watu watatu wameuwawa na wengine 26 kujeruhiwa wakati wa mapambano na wafuasi wa jamii ya Alawite wanaotokana na madhehebu ya Shia.

Picha ya Rais Assad wa Syria ikitiwa moto nchini Lebanon
Picha ya Rais Assad wa Syria ikitiwa moto nchini LebanonPicha: AP

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman