1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kati ya kansela Angela Merkel na rais Sarkozy mjini Berlin

17 Juni 2011

Ujerumani na Ufaransa zimeamua kuwa na msimamo mmoja katika juhudi za kuiokoa Ugiriki.Kansela Merkel na rais Sarkozy wa Ufaransa wanakubaliana hata benki na mashirika ya bima yachangie.

https://p.dw.com/p/11e0b
Kansela Angela Merkel(kulia) na rais SarkozyPicha: picture alliance/dpa

Ufaransa inaonyesha kuachana na msimamo wake wa kupinga kujumuishwa mabenki ya kibinafsi na mashirika ya bima katika mpango wa kuipatia msaada ziada wa mabilioni ya Euro Ugiriki. Hata hivyo, mchango wa sekta hiyo ya kibinafsi unatakiwa uwe wa hiyari .

"Tumepata ufumbuzi wa namna ya kujumuishwa sekta ya kibinafsi tena kwa hiyari-"Amesema rais Nicolas Sarkozy wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari mjini Berlin. Nae kansela Angela Merkel akaongezea :

"Ninasema kinaga ubaga,hakuna misingi ya kisheria hivi sasa inayolazimisha kufanya hivyo, tunasema pia mchango wowote wa wafadhili wa kibinafsi unabidi uandaliwe kwa ushirikiano pamoja na Benki Kuu ya Ulaya ili kuepukana na sintafahamu. Kwa namna hiyo, tunasisitiza ufumbuzi unahitajika haraka ili kueleta hali ya uwazi katika suala hilo."

Dossier Schulden Haushalt Steuern Währung Konjunktur Euro Dossierbild 2
Sarafu ya EuroPicha: picture alliance/dpa

Thamani ya sarafu ya Euro imepanda kulinganisha na Dollar kufuatia makubaliano yaliyofikiwa Berlin kati ya Ufaransa na Ujerumani-wafadhili wawili wakubwa wa Ugiriki.

Mataifa hayo mawili yanataka kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha utulivu wa sarafu ya Euro-amesema hayo kansela Angela Merkel wakati wa mkutano pamoja na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa mjini Berlin:

"Ninataka kusema wazi wazi, ili ieleweke na ninasisitiza kile ambacho daima tumekuwa tukikisema: Euro ndio sarafu yetu ya pamoja. Umoja wa Ulaya na sarafu ya Euro vinategemeana. Ujerumani imefaidika sana na sarafu ya Euro, nguvu zake za kiuchumi, nguvu za kiuchumi za Ujerumani zinashikamana sana na nguvu za sarafu ya Euro na ndio maana tutafanya kila la kufanya kudhamini utulivu wa sarafu ya Euro, na kuhakikisha matatizo yanamalizika."

Angela Merkel und Nicolas Sarkozy in Berlin
Kanasela Merkel na rais Sarkozy wa UfaransaPicha: dapd

Mbali na suala la Ugiriki, kansela Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wamekubaliana umuhimu wa kuzidishwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Syria na kutoa mwito wa kuachiwa huru mwanajeshi wa Israel, Gilad Shalit, aliyetekwa nyara tangu June mwaka 2006 na wanamgambo wa Hamas huko Gaza.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/dapd/afp

Mhariri:Miraji Othman