1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo mapya ya Syria kuanza Machi 23

9 Machi 2017

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura, amesema anakusudia kuanzisha duru nyingine ya mazungumzo kati ya serikali ya Rais Bashar al-Assad na upinzani tarehe 23 mwezi huu wa Machi mjini Geneva.

https://p.dw.com/p/2YrzO
Schweiz Genf Staffan de Mistura
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de MisturaPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

De Mistura ametoa taarifa hiyo kuhusu mazungumzo mapya kati ya serikali ya Syria na upinzani kwa waandishi wa habari mjini New York, akisema duru mpya itajikita juu ya masuala manne muhimu. Masuala hayo ni Utawala, Katiba Mpya, Uchaguzi na Mkakati wa kupambana na Ugaidi, ambao unajumuisha mipango ya kiusalama na hatua za kujengeana imani.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa pande zitakazoshiriki katika mazungumzo mengine mjini Astana, Khazakhstan, ambao utafanyika kabla ya huo unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva tarehe 23 Machi, kuzingatia changamoto zinazoukabili mpango wa kusitisha mapigano. Mazungumzo hayo ya Astana husimamiwa na Urusi, Iran na Uturuki.

Ushindi wa kijeshi ni ndoto ya mchana

Syrien SDF Kämpfer
De Mistura amesema ushindi wa kijeshi kwa upande wowote katika mzozo wa Syria, ni ndoto ya mchanaPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

De Mistura ambaye ameuarifu mkutano wa faragha wa Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa mjini New York amesifu hatua iliyopigwa katika duru ya mazungumzo iliyopita, akisema yaliyofikiwa hayakutarajiwa na kwamba duru inayofuata inapo mahali pa kuanzia. Aidha, amezitaka pande zote katika mzozo wa Syria, kuelewa bayana kuwa hakuna uwezekano wa ushindi wa kijeshi.

''Nimetoa rai kwa wasyria wote, na kwa washirika wao, kuachana na ndoto kuwa bado upo uwezekano wa kushinda kijeshi. Upande huu au ule bado unadhani ushindi huo unawezekana. Ni ndoto, na naweza kuwahakikishieni kwamba najua sababu ya ninayoyasema.'' Ameonya mjumbe huyo.

Staffan de Mistura amesema washiriki katika duru hii ya mazungumzo ambayo itakuwa ni ya mara ya tano watakuwa wale wale walioshiriki katika duru ya nne iliyomalizika tarehe 3 Machi.

Huku hayo yakiarifiwa, majenerali wa Urusi, Marekani na Uturuki wamekutana wiki hii kujadili njia za kuepusha makabiliano baina yao katika operesheni zao ndani ya Syria, na Jumanne jeshi la Urusi lilitangaza kurefushwa hadi tarehe 20 Machi, makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya jeshi la serikali ya Syria na waasi katika kitongoji cha Ghouta Mashariki mwa mji mkuu wa Syria, Damascus.

Raia 14 wauawa katika shambulio la anga

De Mistura ameyasifu mazungumzo hayo na kurefushwa kwa usitishwaji wa uhasama, akisema bila usitishwaji mapigano wa kuaminika, mazungumzo yajayo mjini Geneva yatajikuta katika hali tete.

Taarifa za hivi punde zimeeleza kuwa raia 14, wakiwemo watoto 6 miongoni mwao, wameuawa katika shambulizi la anga, lililofanywa katika kijiji kinachomilikiwa na kundi la IS Kaskazini mwa Syria, na ndege zinazoshukiwa kuwa za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema nchi yake inamuunga mkono de Mistura na mazungumzo anayoandaa, lakini akaongeza kuwa Marekani inadhani kuwa upande muhimu unaokosekana kwenye meza ya mazungumzo, bila hata hivyo kufafanua ni upande gani.

De Mistura amesema yapo mengi ambayo yanaweza kuwa msingi wa makubaliano miongoni wa pande hasimu za wasyria, na kusikitika kuwa suala gumu sasa ni kukubaliana juu ya msingi huo.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe,ebu

Mhariri: Grace Patricia Kabogo