1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo wa kwanza wa kidiplomasia baada miaka 27

Maja Dreyer28 Mei 2007

Leo asubuhi mjini Baghdad, kumeanza mkutano wa kihistoria, yaani baina ya mabalozi wa Marekani na Iran nchini Iraq. Huu ni mkutano wa kwanza wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili baada ya miaka 27. Lengo ni kuzungumzia usalama nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/CB3w
Bandera za Iran na Marekani
Bandera za Iran na MarekaniPicha: AP Graphics

Balozi wa Iran, Hassan Kazemi-Qomi, na mwenzake wa Marekani, Ryan Crocker, nchini Iraq wanakutana sasa hivi katika eneo la ulinzi mkali kati kati ya mji Baghdad ukiwa ni mkutano wa ngazi ya juu ya kabisa kati ya nchi hizo za kiadui tangu miaka 27.

Kabla ya mazungumzo kuanza, waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, alisema ni matumaini yake kuwa mkutano huo ni mwanzo wa sura mpya na ni hatua muhimu kwa eneo zima. “Ninatumai mkutano huo unaleta uelewano wa pamoja na kwamba utafuatiwa na mikutano mingine kwa ajili ya kutatua masuala muhimu", alisema al-Maliki.

Serikali za Iran na Marekani zinalaumiana kwa kuchochea ghasia na mapigano nchini Iraq. Nchi hii kwa sasa imekabwa na mizozo mbali mbali. Pande zote mbili husika katika mkutano wa leo, awali zilisisitiza mazungumo yatahusu suala la usalama pekee. Iran inapinga kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq, vile vile inailaumu Marekani kuwa inawaunga mkono wanamgambo wanaojipenyeza katika mipaka ya Iraq. Marekani inaishutumu Iran kwa kwatumia waasi na wanamgambo wa Iraq silaha kwa njia ya magendo.

Katika hotuba yake kabla ya mazungumzo, waziri mkuu al-Maliki alisema serikali yake inaitaka Iraq iendelee bila ya jeshi la kutoka nje na isiwe kituo kwa makundi ya kigeni ya kigaidi ambayo yanazishambulia nchi jirani. Al-Maliki pia alikumbusha kuwa jeshi la Marekani litabaki nchini mwake kabla halijakamilisha mafunzo kwa polisi ya Iraq.

Balozi Crocker wa Marekani alisema hayatarajii mkutano huo utaleta matokeo ya maana. Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Manouchehr Mottaki aliona lengo la mkutano huo ni kurekebisha sera za wale wanaoikali Iraq pamoja na kulisaidia taifa la Iraq.

Tangu miaka 27 nchi hizo mbili hazina uhusiano wa kidiplomasia. Chanzo cha uadui wao ni utekaji nyara wa raia 52 wa Kimarekani katika ubalozi wa Marekani mjini Teheran mnamo mwaka 1979, muda mfupi tu baada ya kufanyika mapinduzi ya Kiislamu. Raia hao waliachiliwa huru baada ya siku 444 kutokana na Marekani kuahidi kwamba haitajiingiza katika mambo ya ndani ya Iran. Tangu wakati huo, nchi mbili hizo zinabishana hadharani. Nchini Iran, Marekani inaangaliwa kuwa ni shetani kubwa. Na serikali ya Marekani inaiona Iran kuwa moja kati ya nchi ovu zaidi duniani.

Kabla ya mkutano wa leo, hali ya kutoaminiana ilizidi kati ya Iran na Marekani. Marekani ilipeleka meli mbili za kivita kwenye Ghuba ya Uajemi. Iran, kwa upande wake, iliwakamata Wamarekani kadhaa wakitumuhiwa kufanya vitendo vya upelelezi.

Mtaalamu wa Marekani anayejihushisha na Iran, Karim Sadjapoor, anasema kuna mivutano ndani ya serikali zote mbili: “Kuna watu fulani katika serikali za Iran na Marekani ambao hawataki uhusiano kati ya nchi zao uwe bora zaidi. Hata hawakubali kufanyika mazungumzo. Badala yake wanafanya kila wawezalo mazungumzo haya yavunjike.”

Wale wanaoaminika kupinga uhusiano wa karibu zaidi na Marekani katika serikali ya Iran ni wanasiasa wenye msimamo mkali. Nchini Marekani pia, Wahafidhina wakali chini ya naibu rais Dick Cheney, wanaona kuzungumza na adui ni ishara ya udhaifu ambayo haifai. Wale wanaodai sera za Iran ziwe kali na za kijeshi wanakumbusha mzozo juu ya mradi wa kinyuklia wa Iran, kujiingiza Iran katika Iraq na kukamatwa kwa raia wa Marekani.

Kwa hivyo, ni vigumu kwa wale wanaounga mkono mazungumzo, kama vile rais wa zamani wa Iran, Ali Rafsanjani na waziri wa nchi za nje wa Marekani, Condoleezza Rice.