1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani kati ya Waisraeli na Wapalestina yaanza

Dreyer, Maja14 Januari 2008

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka saba wajumbe wa Israel na Palestina leo walikaa meza moja kwa azma ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/CpYC
Suala la Yerusalem ni moja kati ya masuala magumu katika mgogoro huuPicha: dpa

Ilikuwa wiki nne yaanzishwe mazungumzo haya baina ya Israel na Palestina baada ya kutakiwa kufanya hivyo kwenye mkutano wa Annapolis, Makerani hapo mwezi wa Disemba. Wajumbe hao wanaongozwa na waziri wa masuala ya kigeni wa Israel, Bi Zipi Livni kwa upande wa Israel, na waziri mkuu wa zamani wa Wapalestina, Ahmed Qureia. Changamoto inayowakabili ni kubwa: Katika muda wa mwaka mmoja wanatarajiwa kuyatatua masuala magumu zaidi na ya msingi kama vile mipaka, makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, haki za wakimbizi wa Kipalestina, ugawaji wa chemchem za maji na suala la mji wa Jerusalem.


Alipotembelea nchi zote mbili wiki iliyopita, Rais George Bush wa Marekani alisema: "Najua kuwa suala la Jerusalem ni gumu. Kila upande una wasiwasi mkubwa kisiasa na kidini juu ya mji huo. Natambua kwamba kutatuliwa suala hilo kutakuwa changamoto kubwa lakini hiyo ndiyo njia tunayopaswa kupitia."


Waziri Livni na Bwana Kureia walikubaliana kufanya mikutano ya mara kwa mara ili kutafuta mwafaka kwa masuala haya. Baada ya mkutano wa leo, msemaji wa Bi Livni alisema mazungumzo yalifanywa kwa matumaini ya kuendelea mbele. Hata hivyo, kabla ya kuingia mkutanoni, waziri Livni alisema safari hii mazungumzo yatafanyika mbali na vyombo vya habari. Bwana Qureia alisema masuala ya msingi yaligusiwa. "Mazungumzo yalikuwa mazuri na njia bado ni ngumu" - mwisho wa kumukulu.


Yale ambayo hayawezi kukubalika baina ya wajumbe hao yatapelekwa kwenye ngazi ya juu yatatuliwe na waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel na Rais wa mamlaka wa Palestina Bwana Mahmoud Abbas.


Hata hivyo, wote wawili wanakabiliwa na matatizo ya ndani ambayo yanadhoofisha madaraka yao. Kiongozi wa Israel anashinikizwa na vyama viwili vya serikali yake ya mseto. Juu ya hayo, ripoti kuhusu makosa yaliyofanywa na serikali yake wakati wa vita vya Lebanon hapo mwaka wa 2006 inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwezi huu ambayo pengine itasababisha Olmert atakiwe ajiuzulu.


Rais Abbas kwa upande wake anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kundi la Hamas linalodhibiti eneo la ukanda wa Gaza. Afisa mmoja wa Hamas alisema mazungumzo haya na Waisrael ni kitendo cha uhalifu dhidi ya Wapalestina.


Kulingana na maafisa wa serikali ya Israel, Olmert anataka ukubaliwe mfumo ya taifa la Palestina ambalo litatambuliwa pindi Wapalestina wataweza kuhakikisha usalama wa Israel. Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas lakini anataka kuweko mkataba wa amani ambao utamwezesha kulitangaza taifa la Palestina mwishoni mwa mwaka huu.