1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati

26 Septemba 2010

Wasiwasi kuhusiana na hali ya awamu mpya ya mazungumzo Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/PMyF
Benjamin Netanyahu akisaliamiana na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas.Picha: AP

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ameliambia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwamba Israel lazima ichague kati ya amani au ujenzi wake wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, iwapo inataka mazungumzo mapya ambayo mpatanishi mkuu ni Marekani kuendelea. Abbas pia aliishtumu kile alichokitaja kama tabia ya Israel kuendeleza utanuzi wa makazi hayo. Mawaziri wa Israel, wamesema taifa hilo la Kiyahudi litaondoa leo hii ile hatua ya kusitisha kwa muda ujenzi wa makaazi ya walowezi, katika Ukingo wa Magharibi. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amekuwa akijaribu kubadilisha msimamo huo wa Israel ili kuokoa mazungumzo hayo mapya yasisambaratike. Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, wameitaka Israel iongoze muda wa kusitishwa kwa ujenzi huo.

Wakati huo huo, gazeti moja la Kiarabu Al-Hayat limemnukuu Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas akisema kwa sasa hatojitowa mara moja katika mazungumzo ya amani na Israel, hata kama muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, hautoongezwa.

Amesema atashauriana kwanza na taasisi za Kipalestina na Umoja wa Waarabu. Rais Abbas amewasili leo, mjini Paris Ufaransa na atakutana kesho na Rais Nicholas Sarkozy.