1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Makundi ya waasi yajitenga na mazungumzo ya amani

3 Januari 2017

Mpango wa kusimamisha mapigano nchini Syria unaelekea kusambaratika, baada ya makundi mengi ya waasi kusema bayana kuwa yatajitoa katika mchakato wa mazungumo, kutokana na kuendelea kwa hujuma za serikali dhidi yao.

https://p.dw.com/p/2VBKy
Syrien Kämpfe 27.08.2013
Waasi wanasema serikali imevunja makubaliano ya kusitisha uhasamaPicha: Reuters/Afp/Salah Al-Ashkar

Katika tangazo la pamoja makundi hayo ya waasi yamesema yamejitenga na majadiliano yoyote kuelekea mazungumzo ya amani yanayopangwa kufanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana baadaye mwezi huu wa Januari. Sababu iliyotolewa na makundi hayo ni kile yalichokiita 'ukiukaji' wa mpango wa kusitisha mapigano unaofanywa na upande wa serikali.

Waasi wamesema wanaheshimu usitishwaji huo wa mapigano katika maeneo yote ya nchi, na kulalamika kuwa serikali na wanamgambo wanaoiunga mkono hawajaacha kuzishambulia ngome zao. Wamesema serikali imefanya mashambulizi makubwa na ukiukaji wa mara kwa mara wa mpango wa kusimamisha mapigano, hasa katika maeneo ya Wadi Barada na Ghouta Mashariki karibu ya mji mkuu, Damascus.

''Kusonga mbele kwa aina yoyote kunakwenda kinyume na makubaliano ya kusitisha uhasama'', limesema tangazo la waasi, na kuongeza kuwa ikiwa hali hiyo itaendelea makubaliano hayo yatakuwa batili.

Udhaifu wa makubaliano

Syrien Krieg - Soldaten in Aleppo
Waasi wanasema upande wao umekuwa ukiheshimu makubaliano ya kusimamisha mapiganoPicha: picture-alliance/dpa

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika nchi za kiarabu Mohammed al-Omari, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters, akisema mojawapo ya udhaifu wa makubaliano hayo ni kwamba hayakuafikiwa na pande zote za waasi.

''Makubaliano haya ni tete kwa sababu hayawahusishi wote. Wapinzani katika maeneo ya kati na kaskazini yalijiunga nayo, lakini yale kutoka kusini mwa nchi hayakushirikishwa. Mpango wake hauna mkakati wa kuuratibu, na wala hauna uwezo wa kuuchukulia hatua upande utakaojaribu kuyakiuka'' amesema al-Omari.

Mkuu wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman amesema vikosi vya serikali kwa ushirikiano na wanamgambo wa Hizbollah kutoka Lebanon vimesonga mbele katika maeneo ya bonde la Wadi Barada, umbali wa km 15 kutoka Damascus, na kwamba kwa wakati huu vimeingia katika vitongoji vya Ain al-Fijeh, ambako kuna vyanzo muhimu vya maji yanayotumiwa katika mji mkuu.

Hata hivyo, madai kuwa vikosi hivyo vitiifu kwa serikali vimepambana vikali na makundi ya waasi, wakiwemo wapiganaji wa Fateh al-Sham Front iliyokuwa na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida yamekanushwa na upinzani.

Waasi washutumiwa kuhujumu miundombinu ya maji

Syrien Damaskus Wasserkrise
Mamilioni ya wakazi wa mji wa Damascus hawana majiPicha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Serikali imewashutumu waasi kuhujumu miundombinu ya maji, kwa kumwaga mafuta ndani ya maji na baadaye kuyafunga kabisa mabomba. Umoja wa Mataifa umearifu kuwa watu takriban milioni nne waishio mjin Damascus hawana maji tangu tarehe 22 Desemba.

Mpango wa kusitisha mapigano na baadaye kushiriki katika mazungumzo ya kutafuta amani umedhaminiwa kwa pamoja na Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa serikali ya Rais Bashar al-Assad, na Uturuki ambayo inayaunga mkono makundi ya upinzani.

Wakati huo huo, Uturuki imesema imeviharibu vituo vinne vya kundi linalojiita Dola la Kiislamu vilivyo nchini Syria, na kuwauwa wapiganaji 18 wa kundi hilo na kujeruhi wengine 37.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,dpae
Mhariri: Grace Patricia Kabogo