1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Libya yaakhirishwa

6 Januari 2015

Umoja wa Mataifa umeakhirisha mazungumzo ya amani kati ya pande zinazopigana vita nchini Libya.Wakati huo huo ndege za kivita za serikali ya mjini Tobrouk zimeishambulia meli ya mafuta ya Ugiriki iliyotia nanga Derna

https://p.dw.com/p/1EFUb
Picha ya mji mkuu wa Libya Tripoli unaodhibitiwa na wafuasi wa itikaadi kaliPicha: picture-alliance/dpa/Sabri Elmhedwi

Mazungumzo hayo yalikuwa awali yafanyike Disemba tisaa iliyopita,lakini yaliakhirishwa mara kadhaa kutokana na mapigano kupamba moto kati ya vikosi tiifu kwa serikali inayotambuliwa kimataifa na wanamgambo wanaoungwa mkono na makundi ya itikadi kali.

"Mazungumzo yaliyopangwa hayakufanyika" amesema msemaji wa Umoja wa mataifa Stephane Dujarric.Mjumbe wa Umoja wa mataifa Bernardino Leon alizungumza na pande zote ili kusaka ridhaa kuhusu wakati na mahala ya kile kilichokusudiwa kuwa duru ya pili ya mazungumzo kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya nchini Libya.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa,Dujarric ametaja "shida zilizojitokeza katika kutafuta "mahala yanayokidhi masharti ya usalama" kuwa ni miongoni mwa sababu za kuakhirishwa mkutano huo.

Serikali mbili hasimu na mabunge mawili tofauti yanatawala Libya

Miaka zaidi ya mitatu tangu alipong'olewa madarakani na baadae kuuliwa Moammar Ghaddafi katika vuguvugu la mageuzi lililoungwa mkono na nchi za magharibi,Libya ingali bado imezama katika bahari iliyosheheni silaha na makundi ya wanamgambo wenye silaha nzito nzito,na kusimamiwa na serikali mbili na mabunge mawili yanayopingana.

Libyen Brennendes Öllager in Sidra 26. Dez. 2014
Matangi ya mafuta yafuka moto SidraPicha: picture-alliance/dpa/EPA/STR

Bernardino Leon aliwahi kusimamia duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya wabunge wanaohasimiiana katika mji wa Ghadames mwezi septemba uliopita,lakini hakuna matokeo yoyote yaliyopatikana.

Juhudi zake za kuitisha duru mpya ya mazungumzo na kuhimiza mazungumzo mengine sambamba kati ya pande zinazohasimiana zimeshindwa hadi sasa licha ya onyo la baraza la usalama la Umoja wa mataifa lililotolewa mwezi octoba mwaka jana kutaka kuwachukulia hatua,watakaotaka kuvuruga juhudi hizo.

Bunge linalotambuliwa kimataifa limepiga kura wiki iliyopita kutohudhuria mazungumzo yoyote ambayo mahasimu wao walioko Tripoli wataalikwa.

Majirani wa Libya waitaka jumuia ya kimataifa iingilie kati

Wakati huo huo vikosi vya serikali inayotambuliwa kimataifa yenye makao yake makuu mjini Tobrouk,karibu na mpaka na Misri vimeishambulia meli ya mafuta inayoshikiliwa na wafuasi wa itikadi kali katika bandari ya Derna na kuwauwa mabaharia wawili na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Öltanker Araevo Archivbild
Meli ya mafuta ya Ugiriki iliyoshambuliwa kwa mizinga na vikosi vya anga vya serikali inayotambuliwa kimataifaPicha: Aegean Shipping Enterprises Co.

"Visa kama hivi vinadhihirisha umuhimu kwa pande zote kufikia makubaliano-msemaji wa Umoja wa mataifa Stephane Dujarric amesema.

Umoja wa mataifa unasema,tangu mapigano yalipopamba moto,mwezi May mwaka jana,mamia ya raia wa Libya wameuliwa na malaki kuyapa kisogo maskani yao.

Majirani wa Libya wakihofia matumizi ya nguvui yasije yakaenea hadi katika nchi zao,wameitaka jumuia ya kimataifa iingilie kati.Hata hivyo rais Francois Hollande wa Ufaransa amesisitiza uamuzi wowote wa kuingilia kati nchini Libya unabidi upate idhini ya Umoja wa mataifa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga