1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Yemen Hatarini

17 Desemba 2015

Mazungumzo ya amani ya Yemen yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa nchini Uswisi yanazorota kutokana na mvutano kuhusu kuachiwa huru mafisa wa ngazi ya juu wa serikali wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Houthi.

https://p.dw.com/p/1HOyI
Vikosi vya serikali ya Yemen katika mji wa kusini magharibi wa TaizPicha: Reuters

Mazungumzo ya amani ya Yemen yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa nchini Uswisi yanazorota kutokana na mvutano kuhusu kuachiwa huru mafisa wa ngazi ya juu wa serikali wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Houthi.

Mazungumzo kati ya wawakilishi wa serikali na wa wanamgambo wa shiya-Houthi wanaodhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya Yemen,ikiwa ni pamoja na mji mkuu Sanaa yameanza tangu jumanne iliyopita katika mji uliowekwa siri wa Uswisi.

Masaa machache kabla ya mazungumzo hayo kuanza, makubaliano ya kuweka chini silaha yakaanza kufanya kazi nchini humo,lakini kambi mbili zinazohasimiana zimeshaanza kulaumiana kuyaendeya kinyume makubaliano hayo.

Lengo la mazungumzo ya Uswisi ni kusaka namna ya kumaliza mzozo ulioangamiza maisha ya karibu watu 6000 na mamilioni kuyapa kisogo maskani yao tangu Saud Arabia ilipoamua kuingilia kati mwishoni mwa mwezi wa march mwaka huu.

Duru za karibu na mazungumzo zinasema majadiliano ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili yamesitishwa tangu jana usiku.

Juhudi za Upatanishi zimeshika kasi

Wahouthi wamekataa kuwaachia huru,kama wanavyodai wawakilishi wa serikali ya rais Hadi,maafisa kadhaa wa ngazi ya juu ikiwa ni pamoja na waziri wa ulinzi Mahmoud al Subaihi na nduguye rais Hadi,Nasser.Maafisa hao wawili waliokuwa wakiongoza shughuli za upelelezi katika majimbo ya Aden,Lahej na Abyan wanashikiliwa na wanamgambo wa Houthi tangu mwezi Marchi uliopita.Wahouthi wanasema watakuwa tayari kuwaachia huru mara baada ya makubaliano ya kudumu ya kuweka chini silaha,yatakapojadiliwa.

Jemen Waffenpause vor Friedensgesprächen in Genf Mohammed Abdul-Salam
Mkuu wa wajumbe wa Houthi, Mohammed Abdul-Salam,katika mazungumzo ya amaniPicha: Reuters/K. Abdullah

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen,Ismael Ould Cheikh Ahmed wa Mauritania yuko mbioni tangu wakati huo kujaribu kusawazisha mvutano huo.

Zoezi la kuwaachia huru wafungwa linaendelea

Nchini Yemen kwenyewe mapigano yameripuka usiku wa jana kuamkia leo katika eneo la Marib,umbali wa kilomita mia moja toka mji mkuu Sanaa.Watu wasiopungua 15 wameuwawa kutoka pande zote mbili.

UN Genf Friedensgespräche für Jemen Ban Ki-Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na mwakilishi wake maalum,Ismael Ould Cheikh AhmedPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Ndege za kivita zinazoongozwa na Saud Arabia nazo pia zilishiriki katika mashambulio katika mkoa wa Hajja karibu na mpaka wa Saud Arabia.

Katika hali kama hii,zoezi la kubadlishana wafungwa lililofanyika alfajiri kati ya wanamgambo wa Houthi na vikosi vya Kusini,vinavyoshirikiana na serikali ya Hadi,ni tukio pekee la kutia moyo machoni mwa wapatanishi wa kimataifa.

Mashahidi wanasema wahouthi wamewaachia huru wakaazi 265 wa kusini mwa Yemen na badala yake vikosi vya Kusini vikawaachia huru wafuasi 300 wa Houthi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga