1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Yemen yaanza Kuwait

22 Aprili 2016

Mazungumzo ya amani baina ya pande zinazozozana nchini Yemen yameanza nchini Kuwait jana usiku ikiwa ni katika juhudi za kuumaliza mzozo uliodumu mwaka mmoja katika taifa hilo maskini

https://p.dw.com/p/1IafU
Kuwait-Stadt Friedensgespräche mit den Houthi-Rebellen
Picha: Reuters/M. al-Sayaghi

Takribani watu 9,000 wamepoteza maisha yao, thuluthi moja ikiwa ni raia kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo awali yalipangwa kuanza Jumatatu lakini yakacheleweshwa baada ya waasi wa Kishia nchini Yemen wanaofahamika kama Wahouthi na washirika wao kususia kuhudhuria.

Kumekuwa na majaribio ya awali ya kuandaliwa mazungumzo ya amani. Duru hii ya mazungumzo yanayofanyika Kuwait inalenga kutafuta mbinu za kuutatua mzozo baina ya serikali ya Yemen inayotambuliwa na jamii ya kimataifa, na ambayo inaungwa mkono na muungano wa jeshi linaloongozwa na Saudi Arabia, na Wahouthi na washirika wao, ambao wanayajumuisha wanajeshi watiifu kwa aliyekuwa Rais wa muda mrefu Ali Abdullah Saleh.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kuwait Sheikh Sabah al-Khalid al-Sabah, katika hotuba ya ufunguzi aliwaomba Wayemen waachane na vita na kuchagua amani. "Kwa niaba ya Kuwait, serikali yake na watu wake, ni furaha yangu kuwakaribisha ndugu zetu Wayemen katika nchi yao ya pili, Kuwait, kushiriki katika mazungumzo ya Yemen chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa ili kutafuta ufumbuzi wa mzozo. Kupunguza umwagaji damu na kupunguza mateso ya kibinadamu ambayo wamepitia na wanaendelea kupitia"

Jemen Stammestreffen Unterstützer der Huthi Rebellen
Viongozi wa kikabila nchini YemenPicha: picture-alliance/Photoshot/H. Ali

Jumla ya wajumbe 14 kutoka kila upande wanaripotiwa kushiriki katika mazungumzo hayo, ambayo yanasimamiwa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, Ismail Ould Cheikh Ahmed. "Ninawakaribisha kuhudhuria mikutano ya kufikia suluhisho la kisiasa na kuondokana na mzozo huu. Barabara ya amani inaweza kuwa ngumu lakini tunaweza kuitembea. Kuna mitazamo tofauti lakini tunaweza kuwa na mitazamo ya pamoja. Kuna mianya mingi lakini kwa kuwa fikira ni nzuri tunaweza kufaulu."

Siku moja tu kabla ya kuanza mazungumzo hayo, Wahouthi walionya kuwa wangefuta ushiriki wao ikiwa ukiukwaji wa mpango wa kusitisha mapigano ulioanza kutzekelezwa Aprili 10 ungeendelea. Pande zote mbili za mapigano zimeukiuka mpango huo tete.

Jeshi la muungano likiongozwa na Saudia na kuzijumuisha nchi nyingi za Kiarabu – ikiwemo Kuwait, ambayo ni mwenyeji wa mazungumzo hayo – limekuwa likiwalipua Wahouthi tangu mwishoni mwa Machi 2015 kujaribu kuwadhoofisha na kuukamata tena mji mkuu wa Sanaa, baada ya wao kumlazimu kaimu Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi kukimbilia uhamishoni. Tawi la al-Qaeda nchini Yemen liliikamata miji kadhaa pamoja na ukanda wa pwani na kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS, likajiimarisha nchini humo kufuatia vita vya wenywe kwa wenyewe.

Na wakati mazungumzo hayo yakianza Kuwait, wanamgambo wa Houthi na serikali ya Yemen walibadilishana wafungwa katika mji mkuu Sanaa. Jumla ya wanamgambo 71 wa Kihouthi na wanajeshi 50 wa serikali waliachiliwa huru.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Josephat Charo