1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani yaanza Mali

22 Julai 2013

Mazungumzo ya kutafuta amani na maridhiano nchini Mali yanatarajiwa kuendelea leo, ingawa hali ya wasiwasi imeendelea kutanda nchini humo, wiki moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa urais.

https://p.dw.com/p/19BbR
Rais wa Mali, Dioncounda Traore
Rais wa Mali, Dioncounda TraorePicha: picture-alliance/dpa

Mazungumzo hayo kati ya waasi wa Tuareg na Rais wa Mali, Diancounda Traore, na ambayo hayakutangazwa, yameanza jana Jumapili (21.07.2013) mjini Bamako, na kuhudhuriwa pia na wafuasi wa Vuguvugu la kitaifa la ukombozi wa Azawad-MNLA na kundi jingine la Tuareg la baraza la umoja la Azawad-HCUA. Waasi waliohudhuria mazungumzo hayo, ni wajumbe waliosaini makubaliano ya amani na serikali ya Mali, mwezi uliopita.

Mmoja wa wajumbe wa Tuareg, Ibrahim Ag Assaleh, amesema kuwa mazungumzo hayo yalihusu zaidi suala la uwezekano wa kurejea kwa amani na maridhiano, na yanafanyika huku hali ya wasiwasi ikiwa bado imetanda, baada ya bomu la kutengenezwa nyumbani kugundulika katika mji muhimu wa Kidal kabla ya uchaguzi wa tarehe 28 ya mwezi huu wa Julai.

Uchaguzi muhimu kwa Mali

Uchaguzi huo unachukuliwa kama mustakabali muhimu wa baadae wa Mali, ambayo inapambana kurejesha utawala wa kidemokrasia baada ya mzozo wa miezi 18 ulioshuhudiwa kwa mapambano ya waasi wa Tuareg, mapinduzi ya kijeshi na kudhibitiwa kwa nusu ya taifa hilo na makundi yenye itikadi kali za Kiislamu.

Ama kwa upande mwingine katika kuonyesha bado nchi hiyo haina utulivu wa kutosha, kiongozi wa waasi wa Tuareg, alikamatwa kufuatia kitendo cha kutekwa nyara maafisa sita kaskazini mwa Mali, siku ya Jumamosi (20.07.2013). Hata hivyo, maafisa wote hao wameachiwa huru jana. Serikali ya Mali ilililaumu kundi la MNLA kuhusika na utekaji nyara huo, ambao hakuna kundi ambalo hadi sasa limedai kuhusika.

Waasi wa Tuareg
Waasi wa TuaregPicha: picture alliance / AP Photo

Kundi hilo lilichukua udhibiti wa Kidal mwezi Februari, baada ya jeshi lililoongozwa na Ufaransa kuivamia kijeshi Mali, operesheni zilizowaondoa wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Hata hivyo, viongozi wa Mali walifanikiwa kudhibiti tena eneo hilo, baada ya kusaini makubaliano ya amani na makundi ya MNLA na HCUA Juni 18 mwaka huu, kwa lengo ya kuiunganisha tena nchi hiyo na kufungua njia kwa ajili ya kufanyika uchaguzi.

Hali ya wasiwasi bado imetanda

Japokuwa makubaliano hayo yamesainiwa hivi karibuni, lakini waangalizi wana wasiwasi iwapo mji wa Kidal utakuwa tayari kushiriki katika uchaguzi ujao. Mmoja kati ya wagombea kiti cha urais, Tiebele Drame, Jumatano iliyopita, alijiondoa katika kinyang'anyiro hicho, akisema kuwa nchi hiyo bado haijajiandaa vizuri kwa ajili ya uchaguzi, na hasa katika mji wa Kidal.

Mgombea urais aliyejitoa, Tiebile Drame
Mgombea urais aliyejitoa, Tiebile DramePicha: Ahmed Ouoba/AFP/Getty Images

Wagombea wanaopigiwa sana upatu katika uchaguzi huo ni pamoja na Boubacar Keita, waziri mkuu wa zamani wa Mali na Soumaila Cisse, waziri wa zamani na afisa wa juu wa zamani wa Afrika Magharibi. Akizungumza katika kampeni juzi Jumamosi mjini Bamako, Cisse amesema kuwa ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa hila.

Kiongozi wa operesheni za jeshi la Ufaransa nchini Mali, Jenerali Gregoire de Saint-Quentin, amesema Mali bado haina utulivu wa kutosha, licha ya jeshi linaloongozwa na Ufaransa kufanikiwa dhidi ya wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Josephat Charo