1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya ana kwa ana Mashariki ya Kati?

Abdu Said Mtullya10 Agosti 2010

Wapalestina wasema wapo tayari kufanya mazungumo ya ana kwa ana na Israel lakini,

https://p.dw.com/p/OhTb
Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina,Mahamoud Abbas alievaa miwani.Picha: AP

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Wapalestina wapo tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Israel ikiwa nchi hiyo itasimamisha mpango wa kujenga makaazi zaidi ya walowezi wa kiyahudi.

Mahmoud Abbas ametoa kauli hiyo wakati mjumbe wa Marekani wa Mashariki ya Kati George Mitchell anafanya ziara katika eneo hilo.Mahmoud Abbas amesema wapalestina wapo tayari kushiriki katika mazungumzo ya ana kwa ana na Israel ikiwa jopo la pande nne linalosuluhisha katika mgogoro wa Mashariki ya kati linasema hivyo.

Hata hivyo bwana Abbas amewaambia waandishi habari kwamba mazungumzo hayo yatapaswa kufanyika katika msingi wa maamuzi ya jopo hilo yaliyopitishwa tarehe 19 mwezi wa machi.

Bwana Abbas ametoa kauli hiyo katika Ukingo wa Magharibi wakati ambapo mjumbe wa Marekani anaeshughulikia suala la Mashariki ya kati George Mitchell anafanya ziara ya Mashariki ya kati.

Jopo la pande nne linalosuluhisha katika Mashariki ya Kati lilitoa mwito kwa Israel wa kuacha kujenga makaazi mapya ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya wapalestina yanayokaliwa na Israel kwenye Ukingo wa Magharibi na katika Jerusalem ya Mashariki. Jerusalem ya Mashariki ambayo hasa ni maskani ya waarabu ilitekwa na Israel katika vita vya siku sita vya mwaka wa 1967.

Lakini Israel imelikataa pendekezo la kusimamisha ujenzi wa makaazi ya walowezi.Pande zinazosuluhisha katika mgogoro wa Mashariki ya Kati ni Marekani,Urusi, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya. Israel imesema pendekezo la pande hizo nne litavuruga fursa ya kufikia mapatano ya amani.

Mjumbe wa Marekani wa suala la Mashariki ya Kati George Mitchell leo amewasili Mashariki ya Kati na anatarajiwa kukutana na waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa Mamlaka ya wapalestina Mahmoud Abbas na kurejea Marekani hapo kesho.

Waisraeli na wapalestina wamekuwa wanafanya mazungunzo tokea mwezi wa Mei mwaka huu kwa kupitia kwa mpatanishi huyo George Mitchell lakini bado pande hizo hazijafanya mazungumzo ya ana kwa ana tokea kuzuka vita baina ya Israel na Hamas wanaoudhibiti Ukanda wa Gaza kuanzia Desemba mwaka 2008 hadi mwezi Januari mwaka 2009.

Wakati huo huo habari kutoka Jerusalem zinasema Israel imeyakanusha madai ya Hizbollah kwamba Israel ilihusika na mauaji ya aliekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon Rafik Hariri.

Kiongozi wa Hizbollah wa wanamgambo wa kishia alizindua ukanda wa picha zilizodakizwa na ndege za Israel za mahala pa operesheni ya kumuua Hariri. Mauaji hayo yalifanyika mnamo mwaka wa 2005.

Israel imesema madai hayo ni kichekesho.Lakini kiongozi wa kundi la Hizbollah ameilaumu Israel kwa mauaji ya Rafik Hariri na watu wengine 22 tarehe 14 Februari 2005.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE/

Mhariri/ Josephat Charo