1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kusaka amani Mashariki ya Kati yaanza Paris

Sylvia Mwehozi3 Juni 2016

Wawakilishi kutoka nchi karibu 30 wanakutana mjini Paris , kwa lengo la kufufua mazungumzo ya kutafuta amani ya Mashariki ya kati baina ya Israel na Palestina. Hata hivyo hakuna uwakilishi kutoka Israel na Palestina.

https://p.dw.com/p/1Iztg
Frankreich Internationale Nahost-Friedenskonferenz
Picha: Reuters/S. de Sakutin

Wawakilishi kutoka nchi karibu 30 wanakutana mjini Paris Ufaransa , kwa lengo la kufufua mazungumzo ya kutafuta amani ya Mashariki ya kati baina ya Israel na Palestina. Hata hivyo wakati mazungumzo hayo yakianza hakuna uwakilishi kutoka Israel na Palestina. Mazungumzo hayo yanayoongozwa na Ufaransa yanataka kuzileta pamoja pande zote mbili kufuatia jitihada hizo kuvunjika miaka miwili iliyopita.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezishambulia jitihada hizo akisema kwamba mazungumzo ya moja kwa moja pasipo kuwepo na masharti ya awali ni njia pekee ya kupiga hatua katika mgogoro huo ambao umekuwa ajenda kubwa katika mazungumzo kama hayo yaliyopita kwa miongo kadhaa.

Naye waziri mkuu wa Palestina Rami Hamdallah, ametoa wito wa kuwapo na vigezo vya ratiba kali katika utekelezaji wa makubaliano yoyote.

Pia ameonyesha wasiwasi wa matokeo ya moja kwa moja katika mazungumzo na Israel akisema kuwa "tumekuwa na mazungumzo na Israel kwa miaka 20 na hakuna tulichofanikiwa", kauli aliyoitoa mwezi uliopita.

Matumaini ya kupatikana ufumbuzi

Hata hivyo waangalizi wameonyesha kuwepo na matumaini na jitihada mpya za mazungumzo zinazoongozwa na Ufaransa , kwa kuwa malengo yamekuwa ya wastani.

Vyanzo kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa vinasema kwamba lengo ni kuanzisha mchakato utakaozileta upande zote mbili mezani kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Rais wa Ufaransa Francois HollandePicha: Reuters/S. de Sakutin

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault, ambaye alisafiri hivi karibuni kukutana na Netanyahu na viongozi wa palestina , amesema kwamba kuzorota kwa hali ya usalama kunaweka matarajio ya amani kuwa hatarini zaidi.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande akiwasili katika mkutano huo amesema kwamba ; "Ilikuwa ni muhimu kukutana kwa ajili ya jitihada hizi na lengo letu ni moja tu, Amani mashariki ya kati. Mpango huu ni muhimu na kila mtu anatambua hivyo . Ni lazima na muhimu kwa eneo hili , ikiwa bila shaka kazi inayoanza leo itafanyika ipasvyo na kwa malengo . Na hili ndilo alilodhamiria waziri Jean-Marc Ayrault." amesema Hollande.

Wadau wote muhimu waalikwa

Wawakilishi wengine kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na muungano wa nchi za kiarabu, watajaribu kuweka mazingira ya mkutano kamili wa mazungumzo ya amani utakaofanyika mwishoni mwa mwaka.

"Wasiwasi uliopo Ufaransa ni kwamba, hakuna uhakika wa kutatua tatizo kwa njia za kidiplomasia au kisiasa" amesema mmoja ya wanadiplomasia alipozungumza na AFP.

Marekani , kama mpatanishi wa asili katika mgogoro huo , hajaonyesha jitihada za kuzikutanisha pande zote mbili katika mazungumzo ya mani tangu yalipovunjika mwaka 2014.

Tangu mwezi Oktoba wapalestina wameanzisha mashambulizi ya visu dhidi ya waislael wakipinga kukaliwa kwa ukingo wa magharibu na Jerusalem ya mashariki, pamoja na vurugu zinazodaiwa kufanywa na Israel, hata hivyo Isreal mwenyewe anakana madai hayo yote.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA

Mhariri:Iddi Ssessanga