1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kusitisha mashambulizi Gaza yaendelea

12 Agosti 2014

Anga ya Ukanda wa Gaza imesalia tulivu kwa siku ya pili mfululizo ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa saa 72, wakati wapatanishi mjini Cairo wakijiandaa kupambana na suala tete la Israel kuizingira Gaza.

https://p.dw.com/p/1CstF
Gaza Waffenruhe 11.08.2014
Picha: Reuters

Hayo yanajiri wakati Umoja wa Mataifa ukiunda tume ya kuyachunguza maovu yanayofanywa Israel katika Ukanda wa Gaza. Wakati wakaazi wa Gaza wakiendelea na harakati za kujaribu kuyaanzisha maisha yao upya, wajumbe wa Israe na Palestina wanatarajiwa kukutana kwa siku ya pili ya mazungumzo tofauti yanayolenga kufikia suluhisho la kudumu la makabiliano baina yao yaliyodumu wiki tano.

Lakini afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Israel amesema hakuna mafanikio yoyote kufikia sasa, akiliambia shirika la habari la AFP kuwa bado kuna mengi ya kufanywa kabla ya kufikia makubaliano ya kuumaliza mgogoro huo, ambao ulizuka mnamo Julai 8 wakati Israel ilipoanzisha operesheni za kijeshi ili kuzuia mashambulizi ya roketi kutokea Ukanda wa Gaza kuelekea Israel. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 1,940,wengi wao raia, na watu 67 kutoka upande wa Israel, wengi wao wanajeshi.

Saeb Erekat und Nabil Elaraby 11.08.2014 Kairo
Mjumbe wa Palestina Saeeb Erakat (Kushoto) na Mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu Nabil El Araby mjini CairoPicha: Reuters

Mazungumzo ya siku ya kwanza hapo jana yalidumu kwa muda wa saa kumi, huku mjumbe wa Palestina Saeb Erakat akiyataja kuwa “makubwa” lakini akasema ya leo yanatarajiwa kuwa muhimu. "Mtazamo wa Israel katika mazungumzo haya ni wazi: kwamba wamekuja hapa kuongeza mgogoro na kuchochea usaliti. Hawati makubalino ya kusitisha mapigano kwa muda mrefu".

Israel inasisitiza kuwa Hamas wasalimishe silaha zao na mamlaka katika Ukanda wa Gaza, lakini Wapalestina wamekataa. Hamas inaitaka Israel iondoe vizingiti vyote ilivyoweka katika Ukanda wa Gaza katika mwaka wa 2006 kabla ya kukomesha mashambulizi ya roketi. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ansema "Israel haitafanya mazungumzo wakati mashambulizi yakiendelea. Israel itaendelea kufanya kila juhudi kubadilisha hali ya mambo na kurejesha utulivu kwa raia wote".

Amal Alamuddin
Amal Alamuddin amekataa jukumu la kuhudumu katika jopo la kuchunguza maovu ya Ukanda wa GazaPicha: JUSTIN TALLIS/AFP/Getty Images

Pande zote mbili zimesema ziko tayari kuendelea na mashambulizi kama mazungumzo hayo yatakwama tena.

Wakati huo huo, Israel imekasirishwa na hatua ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwateua watalaamu watatu ambao watafanya uchunguzi kuhusiana na mashambulizi ya Gaza.

Mwanasheria wa kimataifa wa Canada William Schabas, ambaye ataiongoza tume hiyo maalum, anaangaliwa na Israel kama adui wa taifa la Kiyahudi kuhuiana na wito wa kumtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu afikishwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu – ICC.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Israel Yigal Palmor amesema mapendekezo ya kuipinga Israel tayari yameandikwa na tume hiyo, na yanasubiri tu sahihi za mwisho. Wengine walioteuliwa katika jopo hilo ni Doudou Diene wa Senegal ambaye aliwahi kuhudumu katika shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi, na wakili wa Lebanon mzaliwa wa Uingereza, Amal Alamuddin. Lakini ripoti zilizotolewa hivi punde zinaarifu kuwa Alamuddin amekataa jukumu hilo alilopewa kuhudumu katika tume hiyo.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu