1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kutafuta amani Yemen yaanza Geneva

15 Juni 2015

Pande zinazozozana Yemen zitakutana kwa mara ya kwanza hii leo Geneva kwa mazungumzo yanayonuia kuutatua mzozo unaosababisha umwagaji wa damu kufuatia mapambano kati ya waasi wa Houthi na wanajeshi wa serikali

https://p.dw.com/p/1FhEu
Picha: picture-alliance/dpa/L. Gillieron

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed amesema kuanza kwa mazungumzo hayo ya leo utakuwa mwanzo wa mashauriano ya awali yanayoshirikisha kila upande kuhusu vita vya Yemen ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,500 na kusababisha mzozo unaotajwa kuwa janga la kibinadamu.

Wachambuzi wanasema kufikiwa makubaliano ni jambo lisilotarajiwa kabisa na hata wajumbe wanaohudhuria mkutano huo unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa hawataanza mazungumuzo wakiwa chumba kimoja.

Kila upande utafanya mazungumzo kivyake

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Ahmad Fawzi amewaambia wanahabari mjini Geneva kuwa badala yake kutaanza mazungumzo ya kila upande kivyake katika vyumba tofauti ambapo mjumbe wa umoja huo atakuwa akiendesha mazungumzo tofauti na kila upande akiwa na matumaini ya kuzishawishi pande hizo kuja katika meza moja ya mazungumzo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Gillieron

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye atahudhuria kikao cha ufunguzi cha mazungumzo hayo amewataka washiriki kushiriki kwa nia njema na bila ya kuweka masharti kabla ya mkutano huo.

Ban amesema mazungumzo hayo yanalenga kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, kukubaliana kuhusu mpango wa waasi wa Houthi kuondoka katika maeneo wanayoyadhibiti na kuongeza juhudi za kutolewa misaada ya kibinadamu.

Yemen imekumbwa na msukosuko kwa miezi kadhaa sasa tangu waasi wa Houthi kuyateka maeneo mengi nchini humo na kumsababisha Rais anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa Abed Mansour Hadi kutorokea uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Saudi Arabia imekuwa ikiziongoza nchi nyingine za kisunni za ghuba kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya waasi Houthi tangu tarehe 26 mwezi Machi lakini zimeshindwa kufikia hadi sasa kuwazidi nguvu waasi hao wa Houthi.

Makundi ya kigaidi yanapata nguvu Yemen

Nchi zenye nguvu zaidi duniani zinataka kuona mzozo huo unakoma kwa kuhofia kupata nguvu zaidi kwa makundi ya kigaidi yenye mafungamano na mtandao wa Al Qaeda nchini humo na katika kanda hiyo kutokana na kutokuwepo utawala thabiti.

Wajumbe wa Yemen wakiabiri ndege mjini Sanaa kuelekea Geneva
Wajumbe wa Yemen wakiabiri ndege mjini Sanaa kuelekea GenevaPicha: picture-alliance/AP Phtot/H. Mohammed

Wawakilishi wa nchi za ghuba, nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Misri, Uturuki, Ujerumani, Uholanzi na Japan pia watashiriki katika mazungumzo hayo.

Umoja wa Mataifa umeutaja mzozo huo kuwa janga la kibinadamu kwani takribani asilimia 80 ya watu Yemen wanahitaji msaada. Huku mazungumzo hayo yakianza, mashambulizi ya angani kutoka kwa majeshi ya Saudi Arabia yameyalenga maeneo ya mashariki na kusini mwa mji mkuu wa Yemen, Sanaa usiku wa kuamkia leo.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel