1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini madogo yaonekana katika mazungumzo ya amani Syria

Mjahida 14 Machi 2016

Mazungumzo ya kujaribu kumaliza mzozo wa Syria yameanza tena mjini Geneva, lakini wakati upinzani ukishindwa kukubaliana juu ya ajenda ya mkutano, kuna matumaini madogo huenda amani ya kudumu ikapatikana

https://p.dw.com/p/1IChH
Schweiz Syrien-Friedensgespräche in Genf
Picha: Reuters/R. Sprich

Mazungumzo hayo yaliosubiriwa kwa muda mrefu, ambayo yameanza tena siku moja kabla ya mgogoro wa nchi hiyo kuingia mwaka wake wa tano, ni ishara ya juhudi za hivi karibuni za kujaribu kusimamisha mapigano yaliyosababisha mauaji ya watu 270,000 huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makaazi.

Saa chache kabla ya mazungumzo hayo kuanza kile kinachokwenda kujadiliwa bado hakikuwa wazi huku mataifa ya Magharibi yakiushambulia utawala wa Syria uliyosema kuwa suala la kumuondoa rais Assad madarakani halitakubalika.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry amesema matamshi hayo kutoka upande wa Syria yanaonesha wazi hatua ya kujaribu kuvuruga mazungumzo na kutuma ujumbe wa vitisho kwa wengine. Kerry ameihimiza Urusi mshirika mkuu wa rais Assad kujaribu kuileta nchi hiyo katika msimamo mzuri huku akisema wakati huu ni wakati ambapo kila mmoja anapaswa kuwajibika.

USA John Kerry in Washington
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: Getty Images/M. Wilson

Hata hivyo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Syria Staffan De Mistura akizungumza na waandishi habari mjini Geneva amesema mazungumzo ya leo ni muhimu na yanahitajika ili kutafuta suluhu ya kisiasa katika mzozo huo unaoingia mwaka wake wa tano. De Mistura amesema iwapo hatoona nia ya kweli majadiliano katika mazungumzo hayo basi atalirejesha suala la Syria kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Misaada ya kiutu yashindwa kupelekwa katika miji minne iliyozingirwa Syria

Huku hayo yakiarifiwa Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu imesema mashirika ya misaada ya kiutu yameshindwa kupeleka misaada katika miji minne iliyozingirwa nchini Syria kutokana na matatizo ya usalama.

Msemaji wa kamati hiyo ya ICRC Pawel Krzysiek amesema kutokana na hali tete ya usalama katika eneo la Qalaat al-Madiq, misaada haiwezi kufikishwa mijini Madaya, Zabadani, Fuaa na Kafraya. Akaongeza "Kila kitu kiko tayari hali ya usalama ikirejea kuwa sawa basi tutaendelea kupeleka misaada katika maeneo hayo."

Syrien Gefecht in Aleppo
Moshi ukifuka kutoka katika majengo yaliyoshambuliwa kwa mabomu mjini AllepoPicha: picture-alliance/dpa/Maysun

Wakati huo huo ripoti mpya iliyotolewa na shirika moja la kitabibu la Syria imedai silaha za kemikali zilitumika mara 161 mwishoni mwa mwaka 2015 nchini humo na kusababisha mauaji ya watu 1,491.

Shirika hilo lililo na makao yake nchini Marekani limeliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na jamii ya kimataifa kufanya haraka kuwakamata wanaotumia silaha hizo na kuwawajibisha kupitia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Mara kwa mara Serikali ya Syria imeshutumiwa na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi kutumia silaha za kemikali dhidi ya watu wake.

Mwandishi:Amina Abubakar/AFP/AP/REUTERS

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman