1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Madagascar yanajadili kuhusu nafasi za juu

Kabogo Grace Patricia26 Agosti 2009

Mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Maputo, Msumbiji yanaongozwa na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano.

https://p.dw.com/p/JIxL
Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano.Picha: AP

Mazungumzo ya awamu ya pili ya kutafuta suluhisho la mzozo wa kisiasa nchini Madagascar yanayofanyika katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, leo yanajadili kuhusu nani ataiongoza serikali mpya ya mpito, kuelekea uchaguzi ujao. Mazungumzo hayo yaliyoanza tena jana yana lengo la kugawana nafasi za juu katika serikali hiyo mpya.

Mazungumzo hayo yanahudhuriwa na viongozi wanaohasimiana Marc Ravalomanana na Andry Rajoelina pamoja na marais wa zamani wa Madagascar, Didier Ratsiraka na Albert Zafy. Chini ya makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kwanza mwanzoni mwa mwezi huu, mahasimu hao wataanzisha serikali ya mpito katika kisiwa hicho kikubwa katika Bahari ya Hindi na kufanya uchaguzi ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao wa 2010.

Chanzo cha habari cha karibu katika mazungumzo hayo yanayoongozwa na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano, kimeeleza kuwa viongozi hao wanne wanaviwakilisha vyama vikuu vya kisiasa nchini humo na kila kiongozi ametoa mapendekezo yake. Chini ya makubaliano yaliyofikiwa Agosti 9, mwaka huu, viongozi hao wanne wanatakiwa wawe wameichagua serikali hiyo ya mpito ifikapo Septemba 8, mwaka huu.

Hakuna mjumbe yeyote katika serikali ya mpito isipokuwa rais wake, ndiyo atakayekubaliwa kugombea katika uchaguzi wa mwakani. Kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Rajoelina, ametangaza kuwa ni yeye pekee ndiyo anaweza kuwa rais wa serikali ya mpito.

Kwa mujibu wa mapendekezo, nafasi nyeti za urais na waziri mkuu huenda zikaangukia kwa Rajoelina. Wafuasi wa chama cha Ravalomanana watapata nafasi za naibu waziri mkuu na spika wa bunge la mpito. Hata hivyo, kiongozi aliyeondolewa madarakani, Ravalomanana amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu alivyoondolewa, na ameahidi kutogombea nafasi ya moja kwa moja katika serikali ya mpito.

Akizungumza kuhusu mkutano huo, Bwana Chissano anasema:

''Bado hatujazungumzia kwa undani kugawana madaraka miongoni mwa wadau tofauti. Tulichokizungumza ni utaratibu wa kulijadili suala hili na sasa tuko mapumzikoni, ili wapatanishi waweze kukusanya yale yote tuliyoyazingatia na baadaye waweze kurudi na mapendekezo mapya.''

Aidha, wapatanishi wa mazungumzo hayo wamesema Bwana Chissano anakabiliwa na kazi ngumu wakati ambao viongozi hao wanagombania nafasi hizo za juu. Leonardo Simao, mjumbe wa wapatanishi kutoka Jumuiya ya Nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), amesema tofauti za viongozi hao haziwezi zikatatuliwa kwa muda wa siku mbili.

Nchi ya Madagascar imekuwa katika machafuko ya kisiasa kuanzia mwezi Machi, mwaka huu, baada ya Rajoelina aliyekuwa meya wa zamani wa Antananarivo kumuondoa madarakani Rais Ravalomanana huku akiungwa mkono na jeshi la nchi hiyo. Kutokana na machafuko hayo ya kisiasa yaliyosababisha vifo vya watu 135, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la ukosefu wa ajira hasa katika maeneo ya mijini.

Mazungumzo haya ya awamu ya pili yanatarajiwa kukamilika jioni hii ya leo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri:M.Abdul-Rahman