1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia yaongezwa muda

Admin.WagnerD30 Juni 2015

Wajumbe wa Iran na wa nchi sita zenye nguvu duniani leo wamerudi tena katika meza ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran mjini Vienna, wakati ikiwa ndiyo siku ya mwisho iliyopangwa kufikiwa makubaliano.

https://p.dw.com/p/1FqpF
Atomverhandlungen in Wien
Waziri wa Mambo ya nje Javad Zarif akiwa katika mazungumzo mijini ViennaPicha: Reuters/C. Barria

Iran na nchi sita zenye nguvu duaniani ambazo ni Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, China, Urusi pamoja na Marekani wamerudi tena katika meza ya mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran leo hii. Pande hizo mbili zimekubaliana mazungumzo kuengezewa muda, ikiwa siku ya mwisho ya kufikiwa makubalaino ilikuwa iwe leo.

Pande zote mbili zinasema zinafahamu kuwa kuna vikwazo vikubwa vya kukabiliana navyo, kabla ya kupata makubaliano ya kudumu.

Makubaliano hayo yatailazimu Iran kupunguza shughuli zake za kinyuklia, ili iweze kuondolewa vikwazo ilivyowekewa kwa zaidi ya muongo moja sasa.

Wanadiplomasia wamesema muda wa mwisho wa kufikia makubaliano kwa hakika sio Juni 30, bali ni Julai 9. Hii ikiwa ndio siku ya mwisho, kwa makubaliano hayo kuwasilishwa katika bunge la Marekani - Congress. Na baada ya kipindi cha siku 30 cha mapitio ya makubaliano hayo, rais Obama wa Marekani ataondoa vikwazo dhidi ya Iran.

Hata hivyo wanadiplomasia hao wamependekeza muda wa mapitio urefushwe hadi siku 60, kuondoa wasiwasi kuwa makubaliano hayo huenda yakavunjwa.

Tafauti kubwa baina ya pande hizo mbili, ni juu ya kasi na muda utakaochukua hadi vikwazo dhidi ya Iran kuondolewa. Pamoja na madai ya nchi za magharibi kuwa lazima Umoja wa Mataifa ufanye ukaguzi wa kambi za kijeshi, pamoja na maabara za wanasanyansi wa teknolojia ya nyuklia. Jambo ambalo Iran hadi sasa hakubaliani nalo.

Nchi za magharibi na Netanyahu waishutumu Iran

Nchi za magharibi na washirika wake wanaishutumu Iran kuwa huenda ikawa inakuza teknologia ya nishati ya nyuklia, ambayo itaiwezesha kuunda silaha za nyuklia. Na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo amesisitiza kuwa mpango unaojadiliwa baina ya Iran na nchi hizo sita, utaipa nafasi nchi hiyo kutengeza silaha za kinyuklia. Hata hivyo Iran inakana shutuma hizo, na kusema shughuli zao za teknologia ya nyuklia ni za salama.

Atomverhandlungen in Wien
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry (katikati)Picha: Reuters/C. Barria

Netanyahu anasema kuinuliwa vikwazo kwa Iran, kutairuhusu kukusanya mabilioni ya fedha na kuiwezesha nchi hio kuendelea na mpango wake wa kigaidi wa kuunda mabomu ya nyuklia.

Maafisa wa Marekani wamesema nchi hizo sita zenye nguvu duniani zitahakikisha kuwa Shrirka la Nishati ya Kinyuklia la Kimataifa (IAEA), linafanya ukaguzi katika maabara za nishati ya nyuklia pamoja na kambi za kijeshi za Iran. Hata hivyo hivi karibuni Kiongozi mkuu wa Iran ayatollah, Ali Khamenei, alisema nchi yake haitokubali maeneo yake ya kijeshi kukaguliwa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman