1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya pande sita yatumbukia mashakani

22 Machi 2007

Mazungumzo ya pande sita juu ya mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini yaonyesha kuwa yamegonga mwamba huku mpatanishi mkuu na washirika wengine wakielekea katika uwanja wa ndege wa Beijing kuelekea makwao.

https://p.dw.com/p/CHHk
Kulia rais Kim Jong ll wa Korea Kaskazini
Kulia rais Kim Jong ll wa Korea KaskaziniPicha: AP

Mazungumzo hayo yamegwaya baada ya Pyongyang kugoma kuendelea kujadiliana juu ya mapatano ya mwezi Februari yaliyoitaka Korea Kaskazini kufunga kinu chake cha nyuklia kufikia katikati ya mwezi wa April hadi pale kiasi cha dola milioni 25 zilizozuiwa kwenye benki ya Macau zitakapo hamishwa na kuwekwa katika benki ya mjini Beijing.

Chini ya makubaliano ya Februari 13 Korea Kaskazini ilikubali kufunga kinu chake cha nyuklia cha Yongbyon kufikia mwezi April na kisha kuwaalika wachunguzi wa umoja wa mataifa kwa mara nyingine tena nchini humo.

Korea Kaskazini kwa upande wake iliahidiwa msaada wa tani elfu 50 wa malighafi za mafuta kwa matumizi yake ya nishati.

Uwekezaji wa fedha hizo umecheleweshwa kwa sababu ambazo hazikuelezwa na wajumbe wa Marekani na Japan wameleezea juu ya kuvunjika kwao moyo kufuatia ucheleweshaji huo na kutofanyika juhudi zozote katika swala hilo.

Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo hayo Christopher Hill alitarajia kuwa uwekezaji wa fedha hizo kutoka benki ya Banco Delta Asia ya Macau hadi katika akaunti ya Korea Kaskazini iliyo katika benki moja ya China mjini Pyongyang ungefanyika kwa haraka.

Mpatanishi mkuu wa mazungumzo hayo ya pande sita wa Korea Kaskazini Kim Kye-gwan hakuzungumza lolote na waandishi wa habari mara tu alipowasili katika uwanja wa ndege wa Beijing na baadae kuondoka na ndege ya shirika la kitaifa la Koryo la Korea Kaskazini kuelekea katika mji mkuu wa Pyongyang.

Lakini rejeo la serikali ya Korea Kaskazini mjini Beijing limeeleza kuwa ujumbe wa Pyongyang umeondoka kutoka kwenye mazungumzo hayo ya pande sita kwa sababu ya kutokuwepo maendeleo yoyote kuhusiana na ahadi ya kuhamishwa fedha hizo, dola milioni 25.

Washington ilitangaza siku ya jumatatu kuwa imekamilisha uchunguzi wake dhidi ya benki ya Macau iliyoshutumiwa awali kuwa iliweka fedha za Korea Kasklazini ambazo zilipatikana kinyume cha sheria ama kupitia utapeli wa kimataifa, hatua iliyosababisha utawala katika eneo la Macau kutwaa mamlaka ya benki hiyo na kudhibiti akaunti hiyo.

Marekani ilitoa ahadi ya kushughulikia swala la fedha hizo kwa muda wa siku 30.

Hadi kufikia sasa hata baada ya muda huo kupindukia fedha hizo bado zimekwama katika benki ya Macau.

Mjumbe wa Urusi Alexander Losyukov nae akiwa njiani kulekea uwanja wa ndege amesema kuwa Huenda benki ya China imekataa kupokea fedha hizo kwa kuhofia kujihusisha na fedha haramu ambazo zinalenga kuinawirisha tena Korea kaskazini.

Kwa sasa Korea Kaskazini haiko tayari kuendeleza mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia na wajumbe wengine wa pande sita wakiwa ni pamoja na Marekani, Korea Kusini, China, Japan na Urusi.

Mazungumzo hayo ya pande sita yalioanza siku ya jumatatu yalitarajiwa kumalizika katika muda wa siku tatu lakini kufuatia sintofahamu hiyo China ambayo ndio mdhamini wa mazungumzo hayo inatarajiwa kutangaza rasmi kuahirishwa kwa mazunguzo hayo baada ya mkutano wa wajumbe uliopangiwa kufanyika jioni leo.