1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya serikali ya mseto Ujerumani

14 Oktoba 2013

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani yumkini wiki hii akamchaguwa mshirika wake mpya katika serikali ya mseto kabla ya kuendelea na mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya Ujerumani katika kipindi kisichozidi miezi miwili.

https://p.dw.com/p/19z7g
Kansela Angela Merkel na Sigmar Gabriel kiongozi wa (SPD).
Kansela Angela Merkel na Sigmar Gabriel kiongozi wa (SPD).Picha: picture-alliance/dpa

Wakati bara zima la Ulaya likisubiri ubayinifu wa msingi wa uchumi wake,Merkel amekuwa akichukuwa hatua taratibu tokea kumalizika uchaguzi wa tarehe 22 Septemba kwa kufanya mazungunmzo ya kufikia makubaliano ya kuunda serikali na mojawapo ya vyama viwili vya kisiasa. Leo anakutana na Chama cha Social Demokratik na hapo kesho anatazamiwa kukutana na chama cha Kijani cha wanamazingira.

Alikuwa na duru ya kwanza ya mazungumzo ya awali wiki iliopita na chama cha SPD ambacho kina viti 194 bungeni na chama cha Kijani chenye viti 63.Hakuna maamuzi yaliofikiwa na hakuna chama kilichoonyesha shauku ya kujiunga naye baada ya mshirika wao wa mara ya mwisho katika serikali ya mseto chama cha kiliberali cha Freedom Demokratik kushindwa kujipatia viti vya kutosha kuweza kuendelea kubakia bungeni.

SPD yadai kima cha chini cha mshahara

Chama kikongwe kabisa nchini Ujerumani cha SPD kimegawika katika suala la ama kukubali au kukataa kujiunga tena na Merkel kuwa mshirika wa serikali ya mseto kutokana na kupoteza wafuasi baada ya kujiunga naye katika serikali ya mseto mwaka 2005 hadi 2009.

Katibu Mkuu wa SPD Andrea Nahles amesema mazungumzo ya leo yatakuwa muhimu sana katika kuamuwa iwapo kuna msingi madhubuti wa kufanya mazungumzo kamili ya kuunda serikali mpya ya mseto.

Katibu Mkuu wa chama cha SPD Andrea Nahles akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin(09.10.2013).
Katibu Mkuu wa chama cha SPD Andrea Nahles akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin(09.10.2013).Picha: dapd

Merkel ameweka wazi uwezekano wa kuunda serikali na chama cha Kijani iwapo chama cha SPD kitasua sua. Viongozi wa chama cha SPD wamewahidi wanachama wake wa ngazi ya chini 472,000 ambao wengi wao wanapinga kuunda tena serikali ya mseto na Merkel fursa ya kuupigia kura uamuzi wowote ule wa makubaliano ya kuunda serikali mpango ambao hauna kifani na unaweza ukawatumbukia nyongo.

Chama cha SPD kinataka kuwepo kwa kima cha chini cha mshahara nchini Ujerumani ambacho kwa sasa hakipo na pia kuwatoza kodi kubwa matajiri madai ambayo yanakataliwa na vyama ndugu CDU cha Merkel na mshirika wao CSU.Chama cha SPD kimesema hapo jana hakuna makubaliano yatakayofikiwa bila ya kuwepo kwa kima cha chini cha mshahara.

Muungano na Kijani kumnufaisha Merkel

Vyama ndugu vya CDU/CSU vitakuwa na mwaziri zaidi na sera zao nyingi kutekelezwa katika serikali ya mseto na chama kidogo cha Kijani ambacho kilishirikiana madaraka na chama cha SPD katika serikali ya mseto mwaka 1998 hadi mwaka 2005 kuliko chama cha SPD.

Kansela Angela Merkel akiwasili kwa mazungumzo na chama cha Kijani mjini Berlin.(10.10.2013).
Kansela Angela Merkel akiwasili kwa mazungumzo na chama cha Kijani mjini Berlin.(10.10.2013).Picha: Reuters

Kwa kuweka wazi uwezekano wa kuunda serikali na chama cha Kijani Merkel anataraji kuimarisha hoja zake katika mazungumzo na chama cha SPD.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu