1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Zimbabwe, mpatanishi aondoka mikono mitupu.

13 Agosti 2008

Mazungumzo juu ya kugawana madaraka nchini Zimbabwe , hayajafanikiwa, pande zote zinavutana.

https://p.dw.com/p/EwFZ
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwasili katika ukumbi wa majadiliano kuhusu mzozo wa kisiasa nchini humo ambapo mazungumzo hayo yanafanyika pamoja na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai.Picha: AP

Mazungumzo juu ya kugawana madaraka nchini Zimbabwe yako katika hali isoyoeleweka bado.Katika mazungumzo hayo bado liko swali juu ya vipi chama cha upinzani cha MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai na chama tawala cha ZANU-PF vinaweza kupata msimamo wa pamoja.

Mpatanishi wa mazungumzo hayo rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki leo ameondoka nchini Zimbabwe akielekea Angola baada ya kupata makubaliano na kundi la chama cha MDC lililojitenga juu ya mazungumzo hayo.

Rais Thabo Mbeki anakwenda nchini Angola kutoa maelezo kwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, rais Jose Eduardo dos Santos, ambapo baada ya kutoa maelezo hayo juu ya maendeleo ya mazungumzo ya Zimbabwe ataelekea nyumbani Afrika kusini.

Mazungumzo hayo yaliahirishwa baada ya rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kufikia makubaliano na Arthur Mutambara, kiongozi wa kundi dogo la chama cha Movement for Democratic Change MDC, ambayo yataelekeza katika uundwaji wa serikali.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Morgan Tsvangirai aliondoka katika majadiliano hayo mapema jana Jumanne akiwa hajaridhika , akionekana kuhisi kuwa anatengwa katika makubaliano ya kumaliza mzozo huo wa kisiasa nchini Zimbabwe. Kiongozi huyo wa chama cha MDC amekuwa akiomba kuahirishwa kwa muda mazungumzo hayo, ili kuweza kutafakari zaidi msimamo juu ya makubaliano hayo. Nae katibu mkuu wa chama cha MDC Tendai Biti amesisitiza juu ya kupatiwa muda zaidi chama hicho kutafakari juu ya makubaliano hayo akieleza kuwa mazungumzo bado hayajafikia mwisho.

Baada ya hapo kulikuwa na uvumi kuwa kungekuwa na mkutano tofauti baina ya Mugabe na kiongozi wa kundi la MDC la Arthur Mutambara. MDC ya Mutambara katika uchaguzi wa mwezi March kimepata wabunge kumi na huenda kundi hilo likasaidia chama cha ZANU-PF cha Robert Mugabe kupata wingi bungeni kwa kuwashirikisha wabunge wake katika chama tawala.

Thabo Mbeki ambaye ni mpatanishi hakutaka kuelezea chochote kuhusu hilo, lakini akasema kuwa iwapo makubaliano ya aina hiyo yatafikiwa, atakuwa amefanikiwa katika majadiliano hayo na kwamba ataweka nguvu zaidi katika majadiliano.

Si hali hiyo tu inayochangia katika uvumi zaidi, lakini pia maelezo ya Mutambara usiku wa jana kuwa atakuwa na mkutano na waandishi wa habari hii leo. Mugabe anataka kubakia kama rais na hakuna uwezekano wa yeye kuachia madaraka, na mpinzani wake Tsvangirai lakini anataka kuwa waziri mkuu na sio kama mshirika mdogo tu wa Mugabe.

Mpatanishi wa mzozo huo Thabo Mbeki hata hivyo hakusema ni lini mazungumzo hayo yataanza tena , kabla ama baada ya mkutano unaoanza mwishoni mwa juma wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya kusini mwa Afrika SADC utakaofanyika mjini Johannesburg.

Mbeki , ambaye ameteuliwa na SADC kupatanisha mzozo huo nchini Zimbabwe, ataufahamisha mkutano huo kuhusu maendeleo ya mazungumzo hayo.

►◄