1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinyo wa nchi za Magharibi juu ya Syria unazidi

Miraji Othman13 Julai 2011

Serekali za nchi za Magharibi leo zilizidisha mbinyo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lichukuwe hatua dhidi ya Syria

https://p.dw.com/p/11uNP
Wafuasi wa utawala wa rais Basahr al-Assad wa Syria wakiandamana mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Damascus kabla ya kuushambuliaPicha: picture alliance/dpa
Wakati huohuo, madarzeni watu walijeruhiwa katika mji wa Zabadani, kusini magharibi ya Syria, wakati majeshi ya usalama yalipoyashambulia maandamano ya amani.

Rais Barack Obama wa Marekani amesema kiongozi wa Syria, Bashar al-Assad, alikuwa hana uhalali baada ya mara kadhaa kuzikwepa nafasi za kuleta marekebisho nchini humo. Aliyasema hayo wakati maingiliano baina ya serekali ya Syria na zile za nchi za Magharibi yanazidi kuzorota baada ya waandamanaji wanaouunga mkono utawala wa Syria kuzishambulia balozi za Marekani na Ufaransa mjini Damascus.

Ufaransa, ambayo pamoja na serekali nyingine za nchi za Magharibi, zimekuwa zikisambaza mswada wa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa miezi sasa, ila zimeona mswada huo ukiwekewa kizingiti na nchi zanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama- nazo ni China na Urusi- imesema ilikuwa muhimu sana kwa taasisi hiyo ya dunia kuchukuwa hatua za kupinga namna Bashar al-Assad anavoukandamiza upinzani. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Gerard Longuet, alisema hilo sio jambo zuri kwa vile Bashar al-Assad anatumia nguvu zisizosemekana kuukandamiza upinzani. Alisema nchi kama vile China na Urusi lazima zifuate kanuni za kawaida, na kwamba mtu hakabiliani na upinzani kwa kutumia moto wa mizinga.

Barack Obama Rede Grundsatzrede Mittlerer Osten Nordafrika
Rais Barack Obama wa Marekani akiikaripia serekali ya Syria kutokana na kushambuliwa ubalozi wa Marekani mjini DamascusPicha: AP

Rais Barack Obama alisema kile ambacho wao wamekiona kutoka upande wa utawala wa Syria ni kipimo cha ukatili kisichokubalika dhidi ya watu wa nchi hiyo. Makundi ya watu yalizishambulia balozi za Marekani na Ufaransa mjini Damascus hapo juzi, jumatatu, baada ya mabalozi wa nchi mbili hizo wiki iliopita kusafiri hadi mji wa Hama, kaskazini mwa mji mkuu, ambako kulikuweko machafuko. Rais Obama aliikaripia serekali ya Rais Assad juu ya shambulio hilo, akisema serekali ya Marekani imetuma risala ilio wazi kwamba hamna mtu atakayeruhusiwa kuuchafua ubalozi wa Marekani na kwamba wao watachukuwa hatua zozote zinazohitajika ili kuulinda ubalozi wao.

Ujerumani nayo ilisema jana kwamba itaunga mkono hatua ya kuliomba baraza la usalama la Mmoja wa Mataifa lipitishe mswada wa azimio litakaloilaani Syria. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema kile kilichotokea mnamo siku chache zilizopita kinaonesha ni muhimu kutolewe tamko la pamoja lilo wazi na la mwisho kutoka jamii ya kimataifa.

Na makamo wa rais wa Syria, Farouk al-Shara, amesema hamna nchi ilio na haki ya kumtaka Rais Bashar al-Asaad ajiuzulu, na hamna mtu ana haki ya kujiingiza katika mambo ya Syria. Alisema Wa-Syria peke yao ndio walio na haki ya kufanya maamuzi kwa ajili yao wenyewe pamoja na Rais Assad ambaye wamemchagua.

Na wakati huo, madarzeni ya watu wamejeruhiwa huko Zabadani, kusini magharibi ya Syria, pale majeshi ya usalama yalipoyasahmabulia maandamano ya amani. Kwanza majeshi ya usalama yalishambulia kwa kutumia hewa ya kutoa machozi.

Mwandishi: Miraji Othman dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman