1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinyo wazidi dhidi ya Assad, msaada wafika Homs

25 Februari 2012

Mataifa ya magharibi na yale ya Kiarabu yameongeza mbinyo dhidi ya serikali ya rais Assad wakati shirika la msalaba mwekundu limesema hatimaye limeweza kuwafikia watu waliojeruhiwa katika mji wa Homs.

https://p.dw.com/p/149ve
Tunisia's Foreign Affairs Minister Rafik Abdessalem (C) addresses the Friends of Syria Conference in Tunis, February 24, 2012. Western and Arab nations meeting on Friday will demand that Syria implement an immediate ceasefire to allow aid in for desperate civilians in the absence of an international consensus on intervention to end a crackdown on an 11-month-old revolt. REUTERS/Jason Reed (TUNISIA - Tags: POLITICS)
Mkutano wa "marafiki wa Syria" nchini TunisiaPicha: REUTERS

Mkutano wa zaidi ya mawaziri wa mambo ya kigeni 60 nchini Tunisia umeshuhudia miito ya kutaka vikosi vya kulinda amani vya mataifa ya kiarabu kuingilia kati na upinzani kupewa silaha , pamoja na onyo lililotolewa na Marekani kuwa Assad atawajibika kwa kiasi kikubwa kwa kudharau utashi wa kimataifa.

Waliojeruhiwa wapatiwa msaada

Katika ishara ya mwanzo kuwa mbinyo unaoongezeka huenda ukawa na athari kwa utawala huo, magari ya kubebea wagonjwa ya shirika la kimataifa la msalaba mwekundu na hilali nyekundu yameingia katika wilaya ya Baba Amr katika mji uliozingirwa wa Homs na kuwaondoa Wasyria saba waliojeruhiwa katika mashambulio ya makombora yaliyofanywa na jeshi la serikali.

Black smoke is seen from Homs refinery February 15, 2012. An explosion hit a major oil pipeline feeding a refinery in Homs, sending a large plume of smoke rising into the sky, witnesses said. The blast hit the pipeline near a district being shelled by government troops, they said. REUTERS/Handout (SYRIA - Tags: CIVIL UNREST POLITICS BUSINESS ENERGY TPX IMAGES OF THE DAY) FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. THIS IMAGE HAS BEEN SUPPLIED BY A THIRD PARTY. IT IS DISTRIBUTED, EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS
Mji wa Homs ukishambuliwa na majeshi ya serikali hivi karibuniPicha: Reuters

Magari matatu ya kubebea wagonjwa yameingia katika eneo la Baba Amr na yameondoka. Yamewaondoa hadi sasa watu saba waliojeruhiwa ambao ni raia wa Syria , msemaji wa shirika hilo la kimataifa la msalaba mwekundu Saleh Dabbakeh ameliambia shirika la habari la AFP mjini Damascus.

Lakini waandishi habari wawili kutoka mataifa ya magharibi ambao wamejeruhiwa bado hawajaondolewa, pamoja na miili ya waandishi habari wengine wawili, ameongeza Dabbakeh.

Majadiliano yanaendelea pamoja na maafisa wa Syria na upande wa upinzani katika juhudi za kuwaondoa watu wote , bila kubagua , ambao wanahitaji msaada wa haraka, amesema.

Vikwazo viongezwe

Mjini Tunis , mkutano wa kwanza wa kile kinachoitwa "marafiki wa Syria", umetoa azimio linalotaka kumalizwa mara moja kwa ghasia na kuwekwa vikwazo vipya.

Kundi hilo limeitaka serikali ya Syria kusitisha mara moja ghasia na matumizi ya nguvu ili kuruhusu makundi ya kutoa misaada kuweza kuwafikia walengwa na kuamua kuchukua hatua za kuweka vizuwizi na vikwazo kwa utawala huo wa Syria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amesema kuwa Assad ajawajibika kwa kiasi kikubwa kwa kudharau matakwa ya jumuiya ya kimataifa.

File Photo. The United States will call for Syria's President Bashar- El Assad to step down. The movie follows attempts to stop El Assad's regime brutality against his people who are seeking democratic reforms. In this Picture Syrian President Bashar Al-Assad during a press conference at the Elysee Palace in Paris, France on July 12, 2008. Photo by Raymond Delalande/JDD/ABACAUSA.COM
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: picture-alliance/abaca

Utawala wa rais Assad umepuuzia kila onyo, na kupoteza kila nafasi , na kuvunja kila makubaliano, Clinton amesema. Ikikabiliwa na maandamano ambayo hayakomi ambapo waandamanaji wanadai haki zao za kimsingi na utu wao, utawala huo unajenga hali ya kutisha ya kiutu.

Msaada wa kiutu

Clinton pia ametangaza msaada wa dola milioni 10 kwa ajili ya juhudi za msaada wa kiutu nchini Syria.

U.S. Secretary of State Hillary Rodham Clinton speaks during a meeting with Japanese Foreign Minister Koichiro Gemba, not pictured, at the State Department in Washington, Monday, Dec. 19, 2011. (AP Photo/Luis M. Alvarez)
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Rodham ClintonPicha: AP

Mjini Washington rais Barack Obama amewaambia waandishi habari ; "Tutaendelea na mbinyo na kuaangalia kila nyenzo inayopatikana kuweza kuzuwia mauaji ya raia wasio na hatia nchini Syria".

Ni muhimu kuwa hatuwi watazamaji tu wakati wa matukio haya yasiyo ya kawaida, ameongeza.

Na huko Syria kwenyewe , kiasi watu 53 zaidi wameuwawa katika ghasia mpya jana Ijumaa, siku mbili kabla ya kufanyika kura ya maoni nchini Syria kuhusu katiba mpya ambayo inaweza kumaliza miaka 50 ya utawala wa chama cha Baath, wakati madaraka makubwa yatakuwa kwa rais.

Tunisia ambayo imekuwa mwenyeji wa mkutano wa mataifa hayo marafiki wa Syria , imetoa wito kwa walinzi wa amani kutoka mataifa ya kiarabu kupelekwa nchini Syria kusaidia kumaliza mauaji, na kwamba Assad apewe kinga ili kumshawishi kuondoka madarakani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Sudi Mnette