1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kupiga kura Somalia waanza

Zainab Aziz23 Septemba 2016

Nchini Somalia uchaguzi wa bunge na wa urais utaanza mwishoni mwa wiki hii kwenye hatua inayolenga kuitoa nchi hiyo kutoka kwenye migogoro ya muda mrefu. Wengi wanaona ndoto hiyo si rahisi kutimia.

https://p.dw.com/p/1K75Y
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais wa Somalia Hassan Sheikh MohamudPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Jebreili

Lengo la rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud la kufanyika kwa uchaguzi katika msingi wa kuwashirikisha watu wote ni la juu sana na si rahisi kutimia. Wengi walililiona kuwa lengo lake lilikuwa na nia nzuri lakini halingeweza kufaulu.

Mwishoni mwa mwaka jana tofauti kati yake na waziri wake mkuu zilijitokeza wazi wazi pia kusuasua kwa mpango wa kurekebisha katiba ya nchi yake na malalamiko ya kisiasa yaliyokithiri kutokana na uwakilishi wa majimbo mbali mbali, vyote hivyo viliashiria kushindwa kutekelezwa kwa azma ya rais Hassan Sheikh Mohamud.

Uchaguzi ujao utawachagua wajumbe 275 wa baraza la wawakilishi na wengine 58 wa baraza la seneti. umuhimu wa koo pamoja na koo ndogo ndogo unatiliwa maanani mno nchini Somalia. Bunge jipya la jamuhuri hiyo litakuwa na mchanganyiko wa jamii kutoka kwenye maeneo mbali mbali kwa mujibu wa mpango wa kugawana mamlaka baina ya koo nchini humo. Hatua hii ni kuwezesha kujiondoa kutoka katika mfumo wa uongozi kutoka kwenye ukoo mmoja kuanzia rais wa nchi, mawaziri hadi wajumbe wanaowakilisha majimbo mbali mbali.

Katika makubaliano mapya vyama vyote vya kisiasa vinahitajika kujisajili halafu wabunge pia wanahitaji kujiunga katika moja wapo ya vyama kufikia Oktoba mwaka 2018.

Wanawake wa Kisomali katika foleni ya kupokea msaada wa chakula
Wanawake wa Kisomali katika foleni ya kupokea msaada wa chakulaPicha: AP

Kufanyika uchaguzi nchini Somalia ni jambo ambalo halikutegemewa hasa kutokana na nchi hiyo kuchukuliwa kuwa ni nchi iliyoanguka huku mashirika ya serikali yakiwa hayana uwezo wa kufanya kazi na pia hali mbaya ya usalama.

Uchaguzi wa mwaka huu jumla ya washiriki 14,025 watachaguliwa hii ikiwa ni idadi kubwa kwa mara mia ukilinganisha na ya mwaka 2012 zoezi ambalo litawahusisha watu milioni 11 tu.

Raia wa Somalia wataraji kuwa uchaguzi huo utatimiza matumaini yao.

Profesa Kenneth Menkhaus mwenyekiti wa kitengo cha maswala ya siasa katika chuo cha Davison nchini Marekani na mfwatiliaji wa karibu wa mambo ya Somalia hafikiriii kama uchaguzi kwa sasa utawezekana, hii ni kutokana na hali mbaya ya usalama pamoja na kutokuwa na uwezekano wa kuyafikia maeneo kadhaa ambayo yako chini ya kundi la Al- Shabaab. Profesa Maenkhaus amesema ''Sidhani kama uchaguzi wa Somalia unaweza kuleta mabadiliko ya muda mrefu katika maendeleo ya siasa za nchi hiyo kama watu wengine wanavyodhani.''

Profesa Menkhaus anakuwa mwangalifu na haamini kwamba uchaguzi ujao utabadilisha mambo nchini Somalia.

Siasa za Somalia hazijabadilika hata baada ya kuwepo mabadiliko kwenye uongozi kwa kuwa mambo bado ni yale yale na bila kujali nani yuko madarakani au katika baraza la mawaziri.

Mchambuzi wa kisiasa nchini Somalia Abdihakim Aynte ameeleza kuwa pamoja na kukabiliwa na matatizo mfumo wa kupiga kura wa Somalia kwa sasa umeimarika kidogo ukilinganishwa na uchaguzi wa miaka minne iliyopita, kuna wajumbe zaidi ya 50 kutoka koo mbali mbali wakiwemo wanawake, vijana, wasomi na wanaharakati huu ni mwanzo mzuri kufwatia hatua ya mwaka 2012.

Uchaguzi huu unaangaliwa kuwa ni hatua itakayoleta mabadiliko na wanachi wa Somalia wanaungojea kwa hamu huku wakiwa na matumaini makubwa.

Mwandishi: Zainab Aziz

Mhariri: Gakuba Daniel