1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo waleta hali nzuri katika uhusiano.

Abdu Said Mtullya17 Julai 2009

Mdahalo wa St Petersburg umeleta mazingira mazuri katika ushirikiano baina ya Ujerumani na Urusi.

https://p.dw.com/p/IrVZ
Wajumbe kutoka Urusi na Ujerumani wakishiriki kwenye mdahalo wa St Petersburg mjini Munic.Picha: DW/Weitz

Ujerumani na Urusi zinazidi kukaribiana tokea rais Medvedev aingie madarakani nchini Urusi. Mgogoro wa uchumi pia unazifanya nchi hizo zinasue masauala yaliyokwama baina yao. Hayo anasema mwandishi wetu, Ingo Mannteufel, katika maoni yake juu ya Baraza la pamoja baina ya Urusi na Ujerumani lililofanyika mjini Munich.

Migogoro ya uchumi na ya fedha inaibadili dunia. Lakini kutambua hayo siyo jambo jipya.Hatahivyo wakati wote ni jambo la kushtusha kuona ni athari zipi zinazosababishwa na katika sekta zipi.

Mabadiliko dhahiri yameonekana kwenye baraza la Urusi na Ujerumani lililofanyika katika mji wa Munich, kufuatia mashauriano yaliyofanyika baina ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Dmitry Medvedev wa Urusi na pia kufuatia mikutano baina wawakilishi wa asasi za kijamii kutoka nchi mbili hizo.

Mashauriano hayo yanafanyika chini ya kinachoitwa "Mdahalo wa St. Petersburg". Mdahalo wa nane , mwanzoni mwa mwezi wa oktoba mwaka jana ulifanyika siku chache kabla ya kufilisika kwa benki ya vitega uchumi - Lehman ya Marekani. Na katika mwezi wa agosti palikuwa na vita vya Georgia, sambamba na tofauti kubwa baina ya Urusi na Umoja wa Ulaya. Palikuwa na hali ya kutoaminiana.

Lakini mdahalo wa safari hii mjini Munich ulikuwa tofauti kabisa. Katika juhudi za kutafuta njia ya pamoja ya kundokana na

athari za mgogoro wa uchumi, uhusiano baina ya Urusi na Ujerumani umekuwa bora. Hata hivyo, haitakuwa sawa kukanusha kwamba bado pana tofauti juu ya masuala fulani baina ya nchi hizo. Lakini pande zote zinatambua kwamba mgogoro uliopo unaweza kutatuliwa kwa juhudi za pamoja tu. Ni kutokana na kutambua hayo kwamba Urusi na Ujerumani zinatekeleza miradi mikubwa ya pamoja ya uchumi- lakini pia zinashirikiana katika sekta nyingine vile vile, kwa mfano katika kutayarisha mwongozo wa masomo ya historia, siku za wandishi habari kutoka kila upande na mpango wa pamoja wa chuo cha filamu.

Mdahalo wa safari hii baina ya Urusi na Ujerumani uliofanyika mjini Munich, umejenga hali ya kuaminiana kutokana na kukabiliwa na mgogoro wa uchumi.

Kielelezo dhahiri ni rais Medvedev. Mikutano mingi ya kimataifa aliyohudhuria imempa uhakika na anazungumza kama jinsi inavyompasa rais wa Urusi. Kwa mfano, ametoa kauli ya uwazi juu ya mkasa wa Natalia Estemirova, mwanaharakati wa haki za binadamu alieuawa. Amelaani mauaji hayo. Msimamo wake unatafautiana na wa rais wa hapo awali Vladimir Putin. Kwenye mdahalo wa mwaka 2006, Putin alijieleza katika njia nyingine juu ya kuuawa kwa mwandishi habari, Anna Politkovskaya. Jee hayo yana maana kwamba uhusiano baina ya Urusi na Ujerumani umekuwa mzuri kutokana na rais Medvedev ? Kwa bahati mbaya siyo kabisa.

Medvedev amechukua hatua fulani kuelekea katika lengo sahihi na ametoa kauli nzuri, lakini utekelezaji unahitajika kutoka upande wake. Watu waliomwuua mwanaharakati wa haki za binadamu na waliomwuua mwandishi habari, lazima wapatikane na wahukumiwe. Kama alivyosema rais Medvedev, watetezi wa haki za binadamu na wandishi habari wanastahili kuungwa mkono na kulindwa. Hayo yatakuwa na manufaa siyo kwa Urusi tu, bali yatasaidia sana katika kuleta ushirikiano mzuri zaidi baina ya nchi hiyo na Ujerumani.

Mwandishi/Mannteufel,Ingo

Mfasiri/Mtullya.