1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo wa wagombea ukansela

14 Septemba 2009

Jana usiku mamilioni ya wapiga kura nchini Ujerumani walitazama televisheni kufuatilia mdahalo kati ya wagombea wawili wa ukansela.

https://p.dw.com/p/JeZa
Angela Merkel Frank-Walter Steinmeier TV Duell Fernsehduell
Wagombea ukansela,Angela Merkel na Frank-Walter Steinmeier.Picha: AP

Majuma mawili kabla ya kufanywa uchaguzi mkuu nchini humu, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wa chama cha CDU na mpinzani wake wa chama cha SPD Frank-Walter Steinmeier walijibu masuala ya waandishi wa habari wanne. Mdahalo huo ulikuwa na umuimu mkubwa sana kwani wapiga kura wengi bado hawakuamua nani wa kumpa kura.

Mdahalo huo ulianza kwa Kansela Merkel na Makamu wake Steinmeier kusifu kipindi walichokuwa wakiongoza serikali. Viongozi hao walifanya kazi pamoja tangu miaka minne iliyopita.Merkel alisema:

"Kwanza inafaa kusema kuwa serikali hii ya muungano wa vyama vikuu kwa kweli imefanya kazi vizuri chini ya uongozi wangu"

Na Steinmeier kwa upande wake alikuwa na haya ya kusema:

"Hapo Bibi Merkel na miye tumeshirikiana ipasavyo. Tumefanikiwa kufanya mengi."

Matamshi yao hayo yaliashiria mkondo utakaofuatwa na mdahalo huo wa dakika 90 : kwa kina na heshima. Yeyote yule alietumaini hatimae kuona mabishano makali katika kampeni ya uchaguzi ambayo hadi sasa haikusisimua, basi alivunjika moyo. Steinmeier aligombea usawa zaidi katika jamii na kima cha chini cha mishahara. Kwa maoni ya mwanasiasa huyo wa SPD, si jambo linaloweza kuruhusiwa kuwa zaidi ya wafanyakazi milioni moja wanaweza tu kuendesha maisha yao kwa kupokea msaada wa fedha kutoka serikalini.

Amesema, mishahara kuendelea kuporomoka ni mkondo unaopaswa kukomeshwa kwani hapo hata hadhi ya kazi ipo hatarini. Mtu anaekwenda kufanya kazi siku nzima anapaswa pia kuwa na uwezo wa kuendesha maisha yake kwa mshahara anaopata-hayo ni mambo yanayokwenda sambamba.

Kwa upande mwingine Kansela Merkel amepigia debe mpango wake wa kiuchumi na azma ya kushirikiana na waliberali wa FDP katika serikali itakayoundwa. Hivi sasa FDP ni chama kikuu cha upinzani katika bunge la Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

Merkel ameeleza waziwazi kuwa sasa anagombea serikali ya muungano mwingine - yaani vyama ndugu imara CDU na CSU vitakavyoshirikiana na FDP katika serikali ya muungano. Anaamini kuwa kiini cha utawala wa miaka minne ijayo, ni kuongeza nafasi za ajira ili kuweza kujitoa haraka katika hali ya sasa ya uchumi unaodorora na kuanza kuimarisha ukuaji wa kiuchumi. Na hayo yanaweza kutekelezwa vizuri zaidi pamoja na FDP. Kwani sera zao zinalingana.

Merkel na Steinmeier walipewa wakati sawa sawa kujibu masuala waliyoulizwa na waandishi wa habari wanne. Masuala hayo hasa yalihusika na mada za uchumi na sera zinazohusika na jamii. Mdahalo ulianza kusisimua kidogo misimamo ya wanasiasa hao ilipotofautiana, kwa mfano lilipozuka suala la nishati ya nyuklia. Merkel anaunga mkono nishati ya nyuklia kinyume na Steinmeier. Kila mmoja aliweza kujitetea vilivyo. Lakini wale waliofuatilizia mdahalo huo kwenye televisheni wanahisi hakuna aliechomoza mshindi dhahiri, hata kama Steinmeier alifanya vyema zaidi katika baadhi ya masuali.

Mwandishi: N. Werkhäuser/ZPR/P.Martin

Mhariri M.Abdul-Rahman