1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MDC yasitisha uamuzi wa kuisusia serikali ya umoja wa kitaifa

Kabogo Grace Patricia6 Novemba 2009

Hayo yameelezwa na kiongozi wa chama hicho Morgan Tsvangirai, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Zimbabwe

https://p.dw.com/p/KPqs
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe (Shoto) akiwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Morgan Tsvangirai (Kulia).Picha: picture alliance/dpa

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha MDC, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Morgan Tsvangirai amesema chama chake kitasitisha uamuzi wake wa kuisusia Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kimempa Rais Robert Mugabe, siku 30 kukamilisha masuala yaliyofikiwa katika mkataba uliosainiwa wa kuundwa serikali hiyo. Tsvangirai ameitoa kauli hiyo mjini Maputo, Msumbiji baada ya mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika-SADC waliyokutana kujadili mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe.

Wito wa viongozi wa SADC

Viongozi hao wa SADC walimtaka Rais Mugabe na Bwana Tsvangirai kurejesha ushirikiano wao kwa manufaa ya nchi yao Zimbabwe. Wiki tatu zilizopita, chama cha Bwana Tsvangirai, cha Movement for Democratic Change-MDC, kilitangaza kusitisha ushirikiano wake na chama tawala cha ZANU-PF cha Rais Mugabe. Chama cha MDC kinakishutumu chama cha ZANU-PF kwa kuhujumu makubaliano yaliofikiwa na kuzuwia mageuzi kuhusu sheria ya vyombo vya habari na mageuzi ya katiba. Lakini mara baada ya mkutano huo wa Maputo Bwana Tsvangirai alisema wamesitisha uamuzi huo.

''Uamuzi ni kwamba tumesitisha kuisusia serikali na kuipa SADC na mpatanishi ambaye ni Komredi Zuma, muda wa siku 15 zijazo kwamba wawakilishi wa vyama watakutana kuangalia masuala yote na jinsi yatakavyotekelezwa na ndani ya siku 30 masuala yote lazima yawe yametatuliwa na kwamba hatutakaa tena kushughulikia mizozo.''

Hata hivyo, pamoja na kwamba MDC ilisusia mikutano yote ya baraza la mawaziri,lakini mawaziri wa chama hicho walikuwa wakiendelea kuziongoza wizara zao. Hatua hiyo ya kuisusia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilizusha wasi wasi kuwa huenda ikairejesha Zimbabwe katika ghasia. Mkutano huo wa SADC ulihudhuriwa na Mfalme Mswati wa Tatu wa Swaziland, Rais Armando Guebuza wa Msumbiji, Rais Rupiah Banda wa Zambia na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, ambao wote kwa pamoja waliwataka viongozi wa kisiasa nchini Zimbabwe kufanya mazungumzo yatakayokuwa na matokeo ya haraka.

Rais Mugabe kwa upande wake anadai ametimiza sehemu yake ya makubaliano na anasisitiza kuwa MDC lazima ifanye kampeni kuhakikisha vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya chama cha ZANU-PF vinaondolewa. Vikwazo hivyo ni pamoja na vizuizi vya kusafiri na misaada ya kifedha.

Msimamo wa nchi za Magharibi

Nchi za Magharibi zimekuwa zikisita kupeleka misaada nchini Zimbabwe hadi hapo serikali ya nchi hiyo itakapokuwa imara katika kuleta demokrasia inayoweza kufanya mageuzi za kisiasa na kiuchumi. Hali ya wasi wasi katika serikali hii mpya ya Zimbabwe ambayo ina miezi minane sasa, ilidhihirika mwezi uliopita wakati mwanaharakati wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa alipokamatwa katika uwanja wa ndege wa Harare na maafisa wa usalama wa Zimbabwe, ingawa alisema alialikwa nchini humo na Waziri Mkuu Tsvangirai.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/DPAE)

Mhariri: Aboubakary Liongo