1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mechi za kirafiki.Ujerumani kutumia chipukizi zaid dhidi ya Sweden

16 Novemba 2010

Leo hii kuna mechi kadhaa za kimataifa za kirafiki, ambapo mahasimu wa kabumbu huko Marekani ya Kusini, Argentina na Brazil, wanapambana nchini Qatar

https://p.dw.com/p/QAWx
Kocha wa Ujerumani Joachim LoewPicha: AP

Ujerumani iko mjini Gothenburg kuumana na Sweden. Joachim Loew ambaye aliongoza kikosi cha vijana wadogo kabisa katika fainali za dunia huko Afrika Kusini,ambacho Ujerumani haijawahi kuwa nacho, hii leo anategemewa kuteremsha dimbani kikosi cha chipukizi zaidi.

 Loew  amewaita katika kikosi chake kwa mara ya kwanza Marcel Schmelzer, mwenye umri wa miaka 22, na Mario Goetze, mwenye umri wa miaka 18, kutoka Borussia Dortmund.Wengine wapya aliyowaingiza kikosini ni chipukizi wawili wa Mainz, Lewis Holtby na Andre Schuerrle.

Mechi nyingine hii leo zitakuwa ni kati ya Uingereza na Ufaransa, majogoo wawili waliyoshindwa kuwika na kutimuliwa mapema kwenye fainali za dunia zilizopita nchini Afrika Kusini.

Ama mabingwa wa dunia, Uhispania, watakuwa mjini Lisbon kucheza na Ureno, mechi ambayo nchi hizo itazitumia kuinadi dhamira yao ya kushirikiana kuandaa fainali za dunia mwaka 2018.

Pambano kati ya Nigeria na Iran limefutwa kutokana na uamuzi wa chama cha soka cha Nigeria, hatua ambayo imekifanya chama cha soka cha Iran kutishia kuishtaki Nigeria kwenye shirikisho la soka duniani, FIFA, kwa hatua yake hiyo.

Malawi itaumana na Rwanda mjini Blantyre, huku Zimbabwe na Msumbiji zikitoana jasho. Ghana wanasafiri hadi Saudi Arabia, kama watakavyofanya Tembo wa Ivory Coast dhidi ya Poland.

Wakati huo huo, kamati ya maadili ya shirikisho la soka duniani, FIFA, leo inatarajiwa kutoa hukumu dhidi ya wajumbe wawili wa kamati ya shirikisho wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa.Hata hivyo, FIFA imesema hukumu hiyo itatangazwa hadharani kesho Alhamisi.

Wajumbe hao, Amos Adamu wa Nigeria na Reynald Temarii wa Tahiti, wanatuhumiwa kuomba rushwa ili kuuza kura zao wakati wa kuchagua wenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2018 na zile za mwaka 2022.

 Kwa muda wa siku tatu kamati hiyo ya maadili imekuwa ikisikiliza ushahidi uliyowasilishwa pamoja na utetezi kutoka kwa wajumbe hao ambao baada ya kuibuka kwa kashfa hiyo wamesimamishwa.

Nchi zinazowania uwenyeji wa fainali hizo za mwaka 2018 ni Ureno kwa kushirikiana na Uhispania, Ubelgiji kwa kushirikiana na Uholanzi, na nyingine ni Urusi, Japan, Korea Kusini Australia, Marekani na Qatar zinawania kuandaa fainali za mwaka 2022.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA/Reuters

Mhariri:Othman Miraji