1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari ya dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika yaanza

15 Juni 2015

Safari ya kufuzu katika dimba la mataifa ya Afrika – AFCON mwaka wa 2017 imeng'oa nanga mwishoni mwa wiki ambapo mechi kadhaa zilichezwa. Ghana iliisambaratisha Mauritius magoli 7-1

https://p.dw.com/p/1FhXp
Ghana Fußball Nationalmannschaft
Picha: F. Leong/AFP/Getty Images

Nayo Nigeria ilikuwa mwenyeji wa Chad mjini Kaduna na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, wakat Afrika Kusini ikishindwa kutamba nyumbani baada ya kutoka sare ya 0-0 na Gambia.

Kwa timu zinazoiwakilisha Afrika Mashariki, Uganda ilipata ushindi wa mabao 2- 0 dhidi ya Botswana, Rwanda ikailaza Msumbiji bao 1-0, nayo Harambee Stars ya Kenya ikatoka sare ugenini ya bao 1-1 na Congo. Burundi ilinyoroshwa na Senegal mabao 3-1, nayo Tanzania ikipata kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Misri katika mechi iliyochezwa jana katika uwanja wa Borg el Arab

CAF haijapokea barua ya kumtaka Blatter asalie

Shirikisho la Kandanda barani Afrika – CAF halijasikia chochote kuhusu mwanachama wake anayemtaka Sepp Blatter kusalia kama rais wa FIFA. Mwanachama wa kamati kuu ya CAF na rais wa Shirikisho la Kandanda la Zambia Kalusha Bwalya amesema hakuna nchi zozote za Afrika zilizowasilisha barua ya kumtaka Blatter aendelee kuhudumu.

Joseph Blatter und Issa Hayatou
Rais wa CAF Isa Hayatou na Rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: picture-alliance/dpa/Messara

Utata unazouzunguka uongozi wa FIFA ulichukua mkondo tofauti jana wakati gazeti moja la USWISI la Schweiz am Sonntag liliporipoti kuwa Blatter mwenye umri wa miaka 79, huenda akasalia kama rais, ikiwa ni chini ya wiki mbili baada ya kuahidi kujiuzulu, siku nne baada ya kuchaguliwa upya.

Ripoti hiyo ilisema Blatter alipokea ujumbe wa kumuunga mkono kutoka kwa mashirika ya kandanda ya Afrika na Asia, yakimtaka atafakari upya uamuzi wake.

Hata hivyo, Domenico Scala, afisa anayesimamia mchakato wa kimchagua rais mpya, amesema jana kuwa kuondoka kwa Blatter ni sehemu ya “lazima“ ya mageuzi yanayopangwa katika shirikisho hilo la kandanda duniani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga